Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SHIRIKA
la Elimu Kibaha, limeingia makubaliano ya kisheria na Kampuni ya
kimataifa ya Organia katika uwekezaji wa ufugaji wa kuku wa kisasa,
utakaoliwezesha shirika hilo kuvuna Sh milioni 100 kwa mwaka na kutoa
ajira kwa watu 700.
Akizungumza
mara baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo jana jioni Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa
Ghasia, alisema uwekezaji huo unatarajiwa kuleta manufaa kwa shirika
hilo kwani uwekezaji wake pia utasaidia kutoa elimu kwa vitendo juu ya
ufugaji kwa kada mbalimbali.
Alisema
miaka ya nyuma shirika hilo lilikuwa likisifika kwa ufugaji wa kuku
kabla ya kusitisha shughuli hizo kutokana na uwepo wa sababu mbalimbali
na kusababisha shirika hilo kukosa mapato yaliyokuwa yakitokana na
uuzaji wa kuku na mayai.
Mkurugenzi
wa Shirika la Elimu Kibaha, Cyprian Mpemba alisema uwekezaji huo wa
miaka 66, mbali na kuingizia shirika hilo kiasi cha Sh milioni 100 kila
mwaka, pia utawawezesha kuvuna kiasi kingine kama hicho kama ada ya
uingiaji katika eneo hilo.
Alisema
itachukua muda wa miaka nane hadi uwekezaji rasmi ukamilike katika eneo
hilo ukihusisha idara mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda vya
usindikaji wa nyama na utengenezaji wa soseji, huku kila baada ya miaka
miwili wakikamilisha ujenzi wa eneo yakiwemo maeneo ya kufugia kuku hao.
Mpemba
alisema matarajio baada ya mika miwili ijayo mradi huo utaweza
kuzalisha kuku milioni 2.7 huku wakitoa ajira kwa watu 120 na
ukikamilika utazalisha kuku milioni 165 pamoja na kutoa ajira kwa watu
700 hatua aliyosema itasaidia kuleta mapinduzi katika ufugaji wa kuku
hapa nchini sambamba na kutoa elimu kwa wanafunzi kutoka vyuo
mbalimbali.
Naye
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Hesham Ewies alisema malengo yao ni
kuibadilisha Kibaha kwa muda mfupi kwa kulifanya kuwa eneo linalosifika
kutokana na shughuli za ufugaji wa kuku huku zaidi wakilenga kuondoa
upungufu wa mahitaji ya bidhaa ya kuku yaliyopo kwa sasa nchini.
Alisema
watarajio yao baada ya miaka michache ijayo, Tanzania itaweza kusifika
kwa usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na kuku kwenda nje ya nchi na
hivyo kuliongeza Taifa mapato.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment