ULEGA: PWANI KITUO KIKUU CHA VIFAA VYA DHARURA KUKABILI EL NINO

WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Mkoa wa Pwani umewekwa kuwa kituo kikuu cha kuhifadhi vifaa vya dharura vitakavyotumika kukabiliana na athari za mvua za El Nino. Amebainisha vituo vingine vimewekwa katika Kanda ya Kati-Dodoma, Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, huku Pwani ikiwa kituo kikuu cha kuhifadhi vifaa hivyo. 

 Ulega ameeleza hayo alipowasili mkoani Pwani kwa ajili ya kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo. 

 Amesema vifaa vilivyohifadhiwa Pwani, vikiwemo makaravati ya chuma, vikapu vya mawe na madaraja ya chuma, vinapaswa kuwa tayari kutumika wakati wowote, huku akisisitiza ukaguzi na usafishaji wa mitaro, makaravati na madaraja ili kuhakikisha maji yanapita kwa uhuru na kuzuia barabara kukatika. 

 Ulega ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania, TANROADS, na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini, TARURA, kuhakikisha wanakagua madaraja na mitaro yote nchini, kuzibua mitaro pamoja na makaravati ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi. 

 Aidha, amezitaka TANROADS na TARURA kufanya tathmini za mara kwa mara katika maeneo hatarishi, akisisitiza tathmini hizo kufanyika kila wiki ili kuongeza nguvu katika maeneo ambayo yanaweza kuzidiwa na mvua na kuhakikisha hakuna barabara inayofungwa. 

 Katika hatua nyingine, amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani kusimamia wakandarasi ambao hawajalipwa, huku akiwataka wakandarasi kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao na kutoa ushirikiano katika kipindi hiki cha maandalizi. 

Meneja wa TANROADS Pwani, Mhandisi Joel Mwambungu, amesema wamejipanga katika mikoa yote 26 inayosimamiwa na TANROADS, ikiwemo kusafisha madaraja, mitaro na makaravati. 

 Ameeleza eneo la Ruvu Chini na Daraja la Mto Mpiji ni miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa kazi, ambapo wanaendelea kusafisha kingo za mto ili kuruhusu maji kupita kwa kiwango kilichosanifiwa. 

 Mwambungu amesema vifaa vilivyopo ni pamoja na makaravati ya chuma yenye urefu wa mita 5,638, sawa na makaravati 568, pamoja na vikapu vipande 4,240, ambavyo vitatumika endapo barabara au madaraja yatapata hitilafu. 

 Amesema pia kuna madaraja makubwa saba, karavati za plastiki zenye urefu wa mita 1,200, sawa na karavati 120, pamoja na karavati za chuma zenye urefu wa mita 1,500, sawa na karavati 150. 

 Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika maeneo wanayoishi, akiwataka wanaoishi mabondeni kuondoka ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.












RC PWANI KUENDELEZA AGENDA YA UWEKEZAJI NA KUWAJENGA VIJANA KIUCHUMI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo, amesema ataendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ili kukuza uwekezaji na uchumi wa Mkoa wa Pwani, huku akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kiuchumi. 

 Mhe. Nyongo amesema hayo leo, Septemba 8, 2026, wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kati yake na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Abubakar Mussa Kunenge, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe. 

 Amesema Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa maeneo muhimu kwa uwekezaji nchini na kwamba atashirikiana na viongozi na wadau mbalimbali kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa rafiki kwa wawekezaji.

 “Mkoa huu ni wa uwekezaji. Nimezunguka maeneo mbalimbali kutafuta wawekezaji, kwa hiyo niwakaribishe kwa kuweka mazingira wezeshi,” amesema Mhe. Nyongo.

MHE. RIDHIWANI KIKWETE AONGOZA MAMIA YA WANANCHI WALIOJIAJIRI KUJIUNGA NA KUJIWEKEA AKIBA NSSF


*Ni katika muendelezo wa kampeni ya elimu kwa umma kuhusu Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri Chalinze mkoani Pwani 

*NSSF yaahidi kufikisha elimu ya hifadhi skimu kwa wananchi wengi zaidi

Na MWANDISHI WETU, PWANI

Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewaongoza mamia ya wananchi wa Chalinze mkoani Pwani, katika muendelezo wa elimu kwa umma kuhusu Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi Waliojiajiri yenye jina la kampeni  "NSSF STAA WA MCHEZO".

Akizungumza na wananchi waliojiajiri, mwishoni mwa wiki iliyofanyika Chalinze mkoani Pwani, Mhe. Ridhiwani ameipongeza NSSF kwa kuja na skimu hiyo ambayo itakuwa mkombozi kwa wananchi waliojiajiri ili kunufaika na mafao ya muda mfupi yakiwemo ya matibabu na mafao ya muda mrefu ambayo ni uzeeni.

Mhe. Ridhiwani amewataka wananchi waendelee kujiunga  na kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye. "Unapojiunga na skimu hii pale unapougua utanufaika na matibabu, ukipata ulemavu utanufaika na mafao ya ulemavu, ukiwa mzee utanufaika na mafao ya uzeeni hivyo ni muhimu kila mwananchi kuchangamkia fursa hii, kwa kujiweka akiba," amesema Mhe. Ridhiwani.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maoni na miongozo yake ambapo kupitia Serikali ya awamu ya sita, wananchi waliojiajiri wanajiwekea akiba NSSF na kunufaika na mafao na huduma nyingine.

"Mpango ulioletwa na NSSF ni kwa ajili ya leo na kesho yako, kwani itafika siku nguvu ya kufanyakazi zitapungua na hapo ndipo NSSF itachukua nafasi ya kuwa Staa wa Mchezo kwa kulipa mafao ya pensheni ya uzee na matibabu," amesema Mhe. Ridhiwani.

Amesema NSSF imeweka utaratibu nzuri wa kujiunga na kuchangia kidogo kidogo kwa siku buku buku, hivyo amewataka wananchi kuendelea kujiunga na kuchangia ili kunufaika na mafao pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na Mfuko.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Omary Mziya, amesema hifadhi skimu inawahusu wananchi waliojiajiri katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi na kuwa inaenda kufungua milango kwa wananchi kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa na NSSF yakiwemo na matibabu. 

Awali,  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Mhe. Hassan Mwinyikondo ameipongeza NSSF kwa kuja na skimu hiyo ambayo itakuwa mkombozi wa wananchi waliojiajiri.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga amemewahakikishia wananchi wa Chalinze na Bagamoyo kuwa mpango huo ni mkombozi kwa wananchi hususani watakapoishiwa nguvu ya kufanyakazi, kwani watapata mafao kutoka NSSF.



 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa