Home » » WANAFUNZI WATAKIWA KUEPUKA VISHAWISHI

WANAFUNZI WATAKIWA KUEPUKA VISHAWISHI

Na Omary Mngindo, Bagamoyo

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete, amewataka wanafunzi wa kike waliopo katika shule za msingi na sekondari, kuepuka vishawishi vinavyoweza kusababisha wakatishe masomo yao.


Alisema wanafunzi wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazochangia wakatishe masomo baada ya kupata mimba na kuolewa hivyo kuharibu malengo yao kielimu na kimaisha.

Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), aliyasema hayo jana katika Mahafali ya kidato cha nne Shule ya Sekondari ya Wasichana Kata ya Mandera.

Katika mahafali hayo, Mama Kikwete aliwakilishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Ummy Ali  Mwalimu.

“Leo wahitimu mnaweka historia kubwa katika shule hii, nyie ndio wanafunzi wa kwanza kuhitimu shuleni hapa hivyo ni vyema mjitahidi kufanya vizuri kwenye mitihani, muwe imara kwa kuhakikisha mnashinda vikwazo vyote mbalimbali,” alisema.

Aliongeza kuwa, Benki ya Dunia imedhamiria kuhakikisha kila mwaka inazuia vifo viwili kati ya wanawake 1,000 ambavyo vinatokana na uzazi.

“Kutokana na tafsiri hii, ndiyo maana Serikali imeweka kipaumbele
cha kuwapatia wananchi wake elimu hasa wasichana ambao ndio walengwa wakuu na janga hili nchini,” alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Rose Umila, alisema ilianzishwa February 28,2009 na wanafunzi 278 kati ya hao 230 ambao waliripoti shuleni, 178 ndio waliomaliza kidato cha nne.

“Changamoto mbalimbali zinazotukabili ni upungufu wa walimu, maabara, madarasa, maktaba, jiko na nyingine nyingi,” alisema.

Kutokaana na changamoto hizo, Bi. Mwalimu aliahidi kumfikishia Mama Kikwete ambaye ndie mlezi wa shule hiyo ili aweze kuzipatia ufumbuzi na hatimaye wanafunzi kupata fursa zote muhimu.
Chanzo: Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa