Home » » MA DC WAJENGEWA UWEZO KUSIMAMIA UTOAJI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10

MA DC WAJENGEWA UWEZO KUSIMAMIA UTOAJI WA MIKOPO YA ASILIMIA 10


 

Na. James Mwanamyoto, OR-TAMISEMI 

 

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale amesema Wakuu wa Wilaya wanapatiwa mafunzo na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ya kuwajengea uwezo wa kusimamia zoezi la utoaji na urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri za Wilaya kwa akina mama, vijana na wenye ulemavu. 

 

Bw. Mtwale amesema hayo leo katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani kwa Niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Bw. Adolf Ndunguru wakati akifungua kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa na Wakuu wa Wilaya zote nchini 

 

Bw. Mtwale amesema, Serikali imeanza kutoa mikopo ya asilimia 10 baada ya hapo awali kusitishwa kutokana na changamoto jilizojitokeza, na kuongeza kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeshapitia kanuni na kufanya maboresho na ikaona ni vema Wakuu wa Wilaya wakapitishwa katika kanuni hizo ili waweze kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa utoaji wa mikopo hiyo. 

 

Tumeona ni vema nanyi mkapitishwa katika kanuni hizo ili tuwe na uelewa wa pamoja katika kusimamia utoaji wa mikopo hiyo ili mikopo hiyo iwe na tija kwa watakaonufaika na katika taifa kwa ujumla, Bw. Mtwale amesisitiza. 

 

Sanjali na hilo, Bw. Mtwale amesema Wakuu wa Wilaya  watapitishwa katika taarifa ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2022/23 ili wafahamu hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwani nao ni wasimamizi wa halmashauri zilizopo katika maeneo yao ya utawala 

 

Ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wakuu wa Wilaya nchini, Bw. Mtwale amesema Ofisi ya Rais - TAMISEMI imemualika mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka ili kuwapatia elimu ya afya ya akili na ya namna bora ya kuepukana na magonjwa ya afya ya akili. 

 

Akiwasilisha mada kuhusiana na afya ya akili, mtaalamu wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dkt. Garvin Kweka amewataka Wakuu wa Wilaya kuzingatia mahusiano ya kijamii ili kujenga afya nzuri ya akili itakayowawezesha kutekeleza kikamilifu majukumu yao kwa ufanisi 

 

Mtu anayeenda kwenye jumuiya, vikoba, kanisani au msikitini akipata msiba, msiba wake hauwi sawa na mtu anayejifungia ndani hivyo mahusiano ya kijamii ni lazima yazingatiwe na kisingi ndio utulivu wa afya ya akili,” Dkt. Kweka amesisitiza. 

 

Kikao kazi hicho cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa na Wakuu wa Wilaya zote nchini, chenye lengo la kuwajengea uwezo kiutendaji viongozi hao kinafanyika kwa siku mbili katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa