Na Gustaphu Haule, Bagamoyo
IMEBAINIKA kuwa wanafunzi wengi wa shule za
sekondari hapa nchini wanashindwa kusoma masomo ya sayansi kutokana na ukosefu
wa maabara, vifaa na wataalamu wa kufundisha masomo ya sayansi.
Hali hiyo ilibainishwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Lugoba, iliyopo wilayani
Bagamoyo, Abdallah Sakasa, wakati akitoa taarifa juu ya maendeleo ya shule yake
katika mahafali ya 21.
Katika taarifa yake alisema moja ya changamoto kubwa iliyoibuka ni pamoja na
ukosefu wa wataalamu wa kufundisha masomo ya sayansi na ugumu wa upatikanaji wa
vifaa vya kufundishia masomo hayo.
Sakasa alisema, changamoto hizo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa
wanafunzi kufanya vibaya mitihani ya sayansi na wengine kukimbia masomo hayo.
"Shule yetu inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo hii ya upungufu wa
viti na meza za kukalia wanafunzi, vitabu, nyumba za walimu na hata maji,
lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa maabara kwa wanafunzi wa sayansi.
“Tunaomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha inasimamia na kuweka
mikakati ambayo itaweza kuinua mchepuo wa masomo ya sayansi hapa nchini ambapo
kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza wataalamu wa masomo hayo,” alisema.
Kwa upande wake Kamishna wa Elimu hapa nchini ambaye alikuwa mgeni rasmi wa
mahafali hayo, Profesa Eustella Bhalalusesa, alisema Serikali ipo katika mpango
wa kuhakikisha inamaliza changamoto zilizopo katika masomo ya sayansi.
Profesa Bhalalusesa alisema kuwa mpango wa kwanza wa Serikali ulikuwa ni
kujenga majengo ya shule pamoja na baadhi ya vyumba vya maabara, lakini mpango
wa pili ni kuhakikisha maabara hizo zinakuwa na wataalamu wa kutosha kwa ajili
ya kufundisha masomo ya sayansi.
Alisema kwa sasa Serikali imeanzisha mafunzo ya walimu wa masomo ya sayansi na
kwamba imepunguza masharti ya kujiunga na masomo hayo hadi katika ngazi ya shahada,
ili kuwafanya wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita kupata unafuu wa kujiunga
na vyuo vya sayansi.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment