na Shehe Semtawa, Bagamoyo
WANANCHI
wa kijiji cha Kitame, tarafa ya Mwambao, wilaya ya Bagamoyo, wameiomba serikali
kuharakisha kuainisha mipaka, ili kupunguza migogoro iliyoko kati yao na
Hifadhi ya Wanyamapori ya Sadani.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwa niaba ya wananchi wenzake mwishoni mwa wiki,
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kitame, Sylivester Kangwe, alisema kumekuwepo na
mgogoro wa muda mrefu wa mipaka kati ya kijiji hicho na hifadhi hiyo, lakini
serikali imekuwa ikisuasua kuimaliza.
Kangwe
alisema migogoro ya mipaka katika eneo lake imekuwa sugu, hali inayosababisha
wananchi kupata adha nyingi ikiwemo kutakiwa kulipa sh 1000 kufika kijiji cha
jirani ambacho nacho hakiko katika eneo la hifadhi.
Wamelitaka
Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (Tanapa) kuondoa kizuizi hicho katika ardhi
ya wananchi, ili wawe huru kutembeleana na kupata huduma muhimu.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, amekiri kupata
malalamiko hayo kutoka kwa wananchi na kudai kuyashughulikia kwa mujibu wa
sheria na hatimaye kuwapatia majibu.
Hata
hivyo, Kipozi akiwa katika ziara ya ghafla katika eneo kilipo kizuizi hicho
alishuhudia wananchi wakitozwa fedha kupita katika kizuizi hicho, hali
iliyomfanya kutoa amri kwa askari wa Tanapa kusitisha suala hilo.
Aliwataka
askari hao kuacha kuwanyanyasa wananchi na kuwapa namba yake ya simu viongozi
wa vijiji vinavyotumia kupita katika kizuizi hicho, ili wampe taarifa endapo
wananyanyaswa na askari hao.
Naye
Ofisa Mipango Miji wa Wilaya ya Bagamoyo, Clemence Mkusa, alisema suala la
mipaka katika vijiji hivyo tayari limeshashughulikiwa na mapendekezo yako
Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment