Baadhi ya washiriki wa warsha ya siku mbili iliyofadhiliwa na Asasi ya Kijamii ya The Foundation for Civil Society ilio lenga kutoa mafunzo kwa maofisa ustawi wa jamii, watendaji kata, kwa kata za Kisiju, Mkuranga na Kimanzichana kupitia mradi wa ‘Kujenga Uwezo wa Asasi’
===== ===== =====
CHAVITA Mkuranga Waomba Kusaidiwa Kielimu
Na Joachim Mushi, Mkuranga
CHAMA cha Viziwi Wilaya ya Mkuranga (CHAVITA), kimeiomba Serikali na wadau wengine kuisaidia jamii hiyo ya walemavu iweze kupata fursa za elimu kama ilivyo kwa makundi mengine na hatimaye kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo kwa sasa wanazikosa.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini hapa na Mweka Hazina wa CHAVITA-Mkuranga, Bi. Subira Upuruje alipokuwa akimsomea risala Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Sila katika warsa ya siku mbili kwa maofisa ustawi wa jamii, watendaji kata, wawakilishi wa vyama vya walemavu na baadhi ya wanachama wa CHAVITA.
Bi. Upuruje alisema watu wenye ulemavu wa kusikia wilayani hapo wapo nyuma kielimu, kwani takwimu zinaonesha kati ya viziwi 200 waliopo eneo hilo ni asilimia 10 tu ndiyo waliopata elimu ya msingi. Alisema hata hivyo wamekuwawakikosa fursa anuai kutokana na kundi hilo kusahaulika, ikiwemo kukosa elimu ya kujikinga na Ukimwi, kutoshiriki katika shughuli za kisiasa na huduma za afya.
“Vituo vya afya vipo hatupati huduma stahili kutokana na wahudumua kushindwa kuwasiliana nasi…wahudumu wa afya hawajui lugha zetu za ishara, hatupati taarifa zozote hata zile elimu za masuala ya kujikinga na Ukimwi. Kwenye siasa tumeshindwa hata kutoa maoni yetu katika mchakato wa Katiba Mpya hapa kwetu, lugha ya alama kwetu ni tatizo,” alisema Upuruje.
Akijibu risala hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bi. Mercy Sila alisema kuanzia sasa ofisi yake ipo wazi hivyo kuwataka makundi hayo kupitia kwa viongozi wao wasisite kumshirikisha katika masuala mbalimbali yanayowatatiza. “…Sasa mlango u-wazi tushirikiane, nami naahidi kuwapa ushirikiano…nawaagiza pia watendaji kata, waratibu na maofisa wengine tufanye hivyo,” alisema B. Sila.
Aliwataka watu wenye ulemavu kutambua kuwa hawajawatenga katika kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. “Kama inatokea kuna sehemu inawakwamisha naomba nipewe taarifa mara moja. Kushiriki katika shughuli za siasa, kijamii na kiuchumi ni haki yenu ya msingi,” alisema Mama Sila.
Aidha alisema sasa umefika wakati wizara ya afya kupeleka watumishi wao wakasome lugha za alama ili kuweza kuwahudumia makundi mengine ya walemavu hasa viziwi. Aliwataka wazazi nao kujifunza lugha hiyo ili waweze kuwahudumia watoto wa aina hiyo kimawasiliano.
Warsha hiyo ya siku mbili iliyofadhiliwa na Asasi ya Kijamii ya The Foundation for Civil Society imelenga kutoa mafunzo kwa maofisa ustawi wa jamii, watendaji kata, kwa kata za Kisiju, Mkuranga na Kimanzichana kupitia mradi wa ‘Kujenga Uwezo wa Asasi’.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com).
0 comments:
Post a Comment