Home » » KAMBI YA MATIBABU VODACOM FOUNDATION YAHAMIA MAGAWA

KAMBI YA MATIBABU VODACOM FOUNDATION YAHAMIA MAGAWA



na Mwandishi wetu, Mkuranga
KAMBI ya kutoa matibabu bure kwa wananchi iliyoandaliwa na Vodacom Foundation, sasa imehamia katika kijiji cha Magawa, wilayani Mkuranga, Pwani.
Wiki iliyopita, mamia ya wakazi wa Kimanzichana wilayani humo walipata huduma za matibabu bure katika kambi hiyo kutoka mpango wa huduma za afya wa Vodacom Foundation.
Kambi hiyo ni mpango wa uboreshaji wa afya wa Vodacom Foundation kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Wanafunzi Tanzania, ambao watatumia utaalamu wao kutoa matibabu.
Akizungumzia kambi hiyo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, alisema Vodacom Foundation imejizatiti kuunga mkono mipango mbalimbali ya afya nchini.
“Taifa lenye watu wenye afya ndilo lenye maendeleo. Wateja wetu ni sehemu ya jamii ya watu hawa ambao wanatuunga mkono na hii ni njia mojawapo ya kipekee ya kuwashukuru,” alisema Meza.
Naye Meneja Ustawi wa Jamii na Elimu, Grace Lyon, alisema wakazi wa kijiji hicho watapata huduma za afya bure kwa magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushauri, vipimo na uzazi wa mpango.
“Watu wengi bado hawana uwezo wa kupata huduma za matibabu na ndio maana tumeshirikiana na taasisi zote za kijamii katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kupitia kambi za afya kama hizi, na pia tunazo njia nyingine za kuunga mkono ujenzi wa hospitali na vifaa vya matibabu maeneo ya vijijini,” alisema.
Aidha Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Namala Mkopi, alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya afya kujitolea kufikisha huduma hizo kwa wananchi wa maeneo ya vijijini ambao bado upatikanaji wa huduma hizo ni changamoto kubwa.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa