Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
WANANCHI wa Kijiji cha Kitame Wilaya ya
Bagamoyo, wameiomba Serikali kuamisha mipaka ya Hifadhi ya Mbuga ya Sadani, ili
kupunguza migogoro iliyopo.
Wakizungumza na waandishi wa habari juzi, baadhi ya wananchi wa kijiji, wameilalamikia
Serikali kushindwa kuainisha mipaka hiyo mapema, hatua inayozua migogoro.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Sylivester Kangwe alikiri kuwapo kwa mgogoro baina
ya wananchi wa kijiji hicho na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Kangwe alisema, licha ya kuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya
utata wa mipaka hiyo, Serikali imeendelea kusuasua katika kumaliza tatizo hilo.
Kangwe alisema, mgogoro wa mipaka katika eneo hilo, umekuwa sugu hali
inayowasababishia kero na usumbufu mkubwa wananchi wa kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Kangwe, wananchi hao hutakiwa kulipa Sh 1000, wanapohitaji kuvuka
kwenda kijiji cha pili kupitia katika hifadhi hiyo.
Kangwe alisema kijiji hicho kipo nje ya eneo la hifadhi, kulingana na mipaka ya
asili na kwamba TANAPA ndiyo walioingia katika ardhi ya kijiji.
“Watu wa hifadhi wameingia katika ardhi ya kijiji na kuweka kizuizi (geti),
wananchi wanashindwa kwenda kupata mahitaji muhimu kijiji cha jirani kutokana
na kuzuizi hiki,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi alikiri kupata malalamiko hayo kutoka
kwa wananchi hao na kudai kuwa malalamiko hayo yanashughulikiwa.
Hata hivyo Kipozi alipiga marufuku wananchi hao kutozwa ushuru huo, pale
alipofanya ziara katika eneo hilo na kukuta wananchi wakilipishwa ushuru huo.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment