Home » » WANANCHI KISARAWE KUANZA ‘KUJAZWA MANOTI’

WANANCHI KISARAWE KUANZA ‘KUJAZWA MANOTI’

Na Mwandishi Wetu, Kisarawe
MBUNGE wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), amesema wananchi wa jimbo lake waliokubali nguzo za umeme zisimikwe katika mashamba yao, ili kuwezesha mradi wa umeme kukamilika, wataanza kulipwa fidia wakati wowote kuanzia wiki hii.

Amesema kuwa, pamoja na kwamba baadhi ya wananchi walikuwa hawaamini kwamba watalipwa fidia kama alivyokuwa amewaahidi, fedha kwa ajili ya malipo hayo, zimeshaingizwa katika akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kwa ajili ya malipo hayo.

Jafo alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akihutubia wananchi katika vijiji tofauti jimboni humo.

Akiwa katika Kijiji cha Msanga, Jafo alisema ili wananchi hao waweze kulipwa fidia yao kwa urahisi, wanatakiwa kufungua akaunti haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za Serikali hazilipwi kupitia madirishani au njia nyingine yoyote tofauti na kupitia benki.

“Kama mtakumbuka nilikuja hapa nikawaambia kwamba, mkubali nguzo za umeme zianze kusimikwa kutoka Kisarawe kuja katika maeneo yenu hata kama fidia hamjalipwa.

“Wapo waliokubali na wengine wakakataa kwa kuhofia kwamba hawatalipwa fidia, mimi nilijitahidi kuwashawishi tena kwa nguvu zote na nashukuru wananchi wangu nyinyi ni waelewa, kwani mlinikubalia na nguzo zikaanza kuwekwa kama mnavyoziona.

“Mliponikubalia hilo, nikaanza kuhangaikia hizo fedha kwa sababu, nilijua kama msipolipwa, basi ubunge wangu utakuwa rehani, lakini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, fedha zote mnazotakiwa kulipwa fidia ambazo ni Sh bilioni 1.2 tayari zimeshawekwa katika akaunti ya halmashauri yetu.

“Kwa hiyo, ninachowaomba wananchi wangu, mfungue akaunti benki, wazee, vijana na akina mama, fungueni akaunti kwa sababu mtaanza kulipwa wakati wowote kuanzia wiki ijayo,” alisema Jafo.

Akiwa katika Kijiji cha Boga, kilichoko Kata ya Manelomango, Jafo alisema baada ya kuingia bungeni, alianza kubuni mbinu za kuwa mbunge wa mfano kutokana na jinsi atakavyokuwa akitatua kero za wananchi kupitia Mfuko wa Jimbo.

“Mara zote nimekuwa nikitumia muda wangu mwingi kuwajali nyinyi wananchi wangu, sasa nawaambia kupitia mfuko huo, tutanunua baiskeli 50 za walemavu na huu ni mwendelezo wa matumizi ya mfuko huu, kwani tayari tumeshajenga zahanati katika Vijiji vya Mlegele, Dololo, tumejenga wodi ya wazazi Manelomango na pia tumejenga ile Shule ya Msingi Jafo.

“Pamoja na mafanikio tunayoyaona, nawaomba sana muache nongwa, acheni fitina kwa sababu baadhi ya watu wamekuwa wakiomba usiku na mchana tusifanikiwe, ili waanze kuchonga kwamba mbunge wenu hana kitu.

“Pamoja na hayo, nawaambia viongozi wote wasiofuata maadili ya kazi waache tabia hiyo, yeyote atakayetaka kukwamisha mradi wowote, huyo nitazaa naye, jamani Jafo kanengahano kayahano (ukinitaka ubaya unanipata),” alisema Jafo na kupigiwa makofi.

Awali, Diwani wa Kata ya Msanga, Abdallah Msese (CUF), na Diwani wa Kata ya Manelomango, Hamis Dikupile (CCM), walimpongeza mbunge huyo na kusema wananchi wanatakiwa kumpa ushirikiano kwa kuwa, amekuwa akichukua kero zao na kuziwasilisha bungeni na kila anaporejea kutoka bungeni, huwafikia wananchi kuwaeleza alichokipata huko.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa