Home » » MGOMBEA AJIVUNIA KIKWETE

MGOMBEA AJIVUNIA KIKWETE

na Julieth Mkireri, Kibaha
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, anayetetea nafasi yake, amerudisha fomu ya kuomba kuchaguliwa tena huku akijivunia kutoa rais wa Tanzania katika kipindi cha uongozi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kukabidhi fomu yake kwa Katibu wa CCM Mkoa, Sauda Mpambalyoto, alisema ameamua kuchukua tena fomu kuendeleza mazuri aliyoyaanzisha.
Mlao ambaye amekuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka 10, alisema anachojivunia katika uongozi wake ni kuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Akielezea mafanikio mengine aliyoyapata katika uongozi wake ni pamoja na kutoa wabunge wote kutoka katika chama tawala tofauti na mikoa mingine ambayo imepata wabunge kutoka vyama vya upinzani.
“Nimechukua fomu kwa mara nyingine kuendeleza yale tuliyoyaanzisha na wanachama wenzangu na pia niendelee kusaidiana nao kukabiliana na changamoto ndani ya chama chetu, ili kiweze kuwa na mwonekano mzuri tofauti na wengine wanavyofikiria,” alisema Mlao.
Aidha, alisema wakati wa uongozi wake amekumbana na changamoto ya mgogoro wa wakulima na wafugaji ambao umesababisha kupoteza maisha ya wananchi, hali ambayo inamuumiza katika kipindi chake cha uongozi.
Alisema kuwa pamoja na kuwa changamoto hiyo inatatuliwa na serikali, lakini pia inakihusu chama hicho tawala.
Changamoto nyingine ni ya jiografia ya mkoa huo ambayo inawalazimu kutumia ndege kufika katika Wilaya ya Mafia na pia ukubwa wa Wilaya ya Bagamoyo na Rufiji ambazo zinahitaji muda mrefu kuzifikia.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa