Home » » WALIMU WAKUU WATAHADHARISHWA

WALIMU WAKUU WATAHADHARISHWA

na Victor Masangu, Pwani
WAKUU wa shule za sekondari nchini wametakiwa kuacha tabia ya kusajili wanafunzi ambao hawajapata nafasi ya kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari kwa kigezo cha kuziba nafasi ya wale waliochaguliwa na kushindwa kuripoti.
Wito huo ulitolewa jana na mwakilishi wa Mkaguzi Mkuu wa Shule za Sekondari Kanda ya Mashariki, Paulo Mosha, alipokuwa akifungua mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Kanda ya Mashariki (TAHOSSA) uliofanyika kwenye Ukumbi wa JKT Ruvu, Mlandizi wilayani Kibaha.
Mosha alisema, Ofisi ya Mkaguzi wa Elimu Kanda ya Mashariki imebaini kuwapo kwa wanafunzi wengine shuleni wakati hawajafaulu na wameingizwa kinyume na taratibu.
“Kwa kweli, napenda kuwaasa wakuu wa shule kuwa makini na kufanya utafiti wa kina kupitia tena upya usahihi wa wanafunzi waliopo shuleni, kwani imebanika kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wapo shuleni na wanaendelea na masomo lakini si halali.
“Naomba hili jambo tusilifumbie macho, kwani inasikitisha kukuta kuna wanafunzi wengine wanajiunga bila ya kufuata taratibu na kanuni, na pindi unapombaini na kumuuliza anasema amepatiwa nafasi kupitia Mwalimu Mkuu,” alisema Mosha.
Mbali ya hilo, aliwataka walimu wakuu hao wasikwepe majukumu yao ya kila siku hasa wanapopangwa kusimamia vituo mbalimbali vya mitihani.
Naye Mwenyekiti wa umoja huo, William Ngullo, alisema mkutano huo una lengo la kupunguza wanafunzi wanaofanya vibaya katika mitihani yao na kuweka mikakati ya kuongeza idadi kubwa ya wanaofaulu.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa