Home » » WAJASIRIAMALI WALILIA SOKO KUTANGAZA BIDHAA

WAJASIRIAMALI WALILIA SOKO KUTANGAZA BIDHAA



na Julieth Mkireri, Kibaha
WAJASIRIAMALI katika Halmashauri ya mji wa Kibaha, mkoani Pwani, wamelalamikia ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa zao, hali inayochangia kufanya biashara kwa hasara.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana, walisema tatizo la kukosa eneo maalumu la kutangaza na kuuza bidhaa wanazotengeneza limekuwa likiwasababishia hasara kutokana na kusafiri umbali mrefu kusaka wateja.
Walisema kuwa soko lililopo ni la wafanyabiashara wa kawaida na haliwanufaishi wale wanaosindika bidhaa mbalimbali hususan za unga wa muhogo, mboga za majani, jam na bidhaa nyingine.
Walisema wamekuwa wakitumia zaidi ya sh 2,000 kusafiri kwenda Kariakoo, Dar es Salaam kupeleka bidhaa zao ambazo huziuza kati ya sh 700 hadi 3,000 kulingana na bidhaa waliyotengeneza.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba serikali ya wilaya hiyo kuwaandalia eneo maalumu la kuuza na kutangaza bidhaa zao kama ilivyo kwenye maeneo mengine mbali na mji huo.
Kwa upande wake Jesca Felix (30 anayejishughulisha na usindikaji wa unga wa muhogo na mboga za majani, alisema soko limekuwa ni changamoto kubwa inayowasumbua kwa muda mrefu ambayo hadi sasa haijapatiwa ufumbuzi.
Alisema ombi hilo la kuwepo na soko wamekuwa wakilitoa kwenye maonesho mbalimbali ya biashara, lakini halijapatiwa ufumbuzi jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwao.
“Sisi wajasiriamali wa mji wa Kibaha tunaona kama serikali haituthamini kwakuwa kero yetu ya muda mrefu ya kupata eneo la kuuzia bidhaa zetu halijapatikana, inatulazimu kuzungukia wateja maofisini kuwauzia bidhaa zetu bila hivyo tutaendelea kukaa nazo kwa muda mrefu bila kuziuza,” alisema mjasiriamali huyo.
Aidha, kwa upande wake, Monica Muya (28) alisema kuwa wakati mwingine wanapotengeneza bidhaa zao hususan za usindikaji wa unga wa muhogo, utengenezaji wa jam na mafuta ya nazi inawalazimu kusafiri hadi Kariakoo jijini Dar es Salaam kushiriki kwenye maonyesho ya kibiashara yanayofanyika katika maeneo mbalimbali ili waweze kutangaza na kuuza bidhaa wanazotengeneza.
Akizungumzia suala la soko, Mkurugenzi wa mji huo, Jenifa Omolo, alisema mji huo uko kwenye utaratibu wa kuendelezwa ambapo kila kitu kitakuwa kwenye mpangilio, hivyo suala la soko pia litapatiwa utatuzi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa