Home » » TANROADS WAPIGWA MARUFUKU KUTUMIA SIMU ZA MIKONONI

TANROADS WAPIGWA MARUFUKU KUTUMIA SIMU ZA MIKONONI

Na Gustaphu Haule, Kibaha
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Greyson Lwenje, amewapiga marufuku wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) waliopo katika vituo vya mizani kuacha kutumia simu zao za mikononi, kwa kuwa zinachangia kuwapo kwa vitendo vya rushwa.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi, wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya barabara, inayojengwa Pwani ambapo pamoja na kukagua miradi hiyo, alitembelea mizani iliyopo Kibaha na kuwataka wafanyakazi hao kuacha kutumia simu zao za mikononi.

Alisema simu za mikononi zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa vitendo vya rushwa vinavyofanywa baina ya wafanyakazi wa mizani, madereva na hata matajiri mbalimbali wanaosafirisha mizigo, jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kazi.

Kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo, alisema kwa sasa hakuna ruhusa kwa wafanyakazi wote wa mizani kuingia na simu zao za mikononi na badala yake wanatakiwa kuhakikisha wanaziacha simu hizo nje, huku zikiwa zimezimwa.

“Wafanyakazi wa mizani wamegundulika kufanya vitendo vya rushwa kupitia simu zao za mikononi kwa kuwasiliana na madereva na hata matajiri wa magari hayo, lakini kuanzia leo hakuna ruhusa kwa mfanyakazi yeyote kuingia mizani akiwa na simu,” alisema Lwenje.

Alisema mfanyakazi atakayebainika kukutwa na simu katika maeneo ya mizani ni lazima achukuliwe hatua kali za kisheria, ikiwamo kufukuzwa kazi.

Alimtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Tumaini Sarakikya, kuhakikisha anawaandikia barua wafanyakazi hao za kuwataka waache kubeba simu zao pindi wakiwa katika mazingira ya kazi.

Akiwa mkoani Pwani, alitembelea Barabara ya Bagamoyo-Msata, yenye kilomita 64 na ile ya Ndundu-Somanga zinazojengwa kwa kiwango cha lami ambapo pamoja na mambo mengine, aliwataka wakandarasi wa barabara hizo kujenga kwa kiwango kinachokubalika.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa