Home » » MBUNGE WA CHALINZE AUTAKA UENYEKITI WA WAZAZI

MBUNGE WA CHALINZE AUTAKA UENYEKITI WA WAZAZI

Na Mwandishi Wetu, Chalinze
MBUNGE wa Chalinze, Said Bwanamdogo, amejitosa katika kinyang’anyiro cha kuomba kuteuliwa kugombea Uenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza mjini hapa jana, alisema moja kati ya dhumuni la kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni kuendelea kupambana na changamoto alizokutana nazo wakati akiwa mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Taifa ya chama hicho.

“Baada ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji kwa kipindi kinachomalizika sasa, nimepata uzoefu mkubwa wa kukabiliana nazo na ndio maana nimeingia katika kinyang’anyiro hicho na hatimaye niendeleze mapambano hayo.

“Moja ya changamoto nilizozikuta wakati nikiwa mjumbe wa kamati hiyo ni deni kubwa la NSSF kwa wafanyakazi wa jumuiya yetu. Tulikubaliana kuanzia kipindi cha uongozi wetu kuanza kulipa malimbikizo ya deni hilo. Katibu Mkuu ambaye ndiye mtendaji wetu chini ya usimamizi wake alihakikisha kulipwa kwa deni hilo kila mwezi,” alisema Bwanamdogo.

Alisema endapo atachaguliwa ataendelea kuyasimamia mafanikio yote yaliyopatikana katika kipindi chote cha uongozi unaomaliza muda wake.

Alisema atasimamia na kuanzisha nafasi za uwakilishi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na bungeni.

Alisema kwa kuwa Jumuiya hiyo haina Baraza la Wadhamini, akichaguliwa atasimamia uanzishwaji wake.

“Kwa muda mrefu Jumuiya yetu haina Baraza la Wadhamini, hivyo nitasimamia uanzishwaji wake mapema iwezekanavyo kwa kuwa chombo hicho ni muhimu kwa uendelezaji na ulinzi wa mali za jumuiya,” alisema Bwanamdogo.

Alisema akichaguliwa atazidi kuboresha shule za Jumuiya hiyo na kuanzisha vyuo vya ufundi, kilimo na biashara.

Aidha, alisema akichaguliwa atayapatia ufumbuzi madai mbalimbali ya wafanyakazi wa Jumuiya hiyo kama vile malimbikizo ya mishahara, nauli za likizo, madeni mbalimbali ya wastaafu na waliohamishwa.

Alisema atasimamia uanzishwaji wa Family Benki ambayo imeonyesha kuingia ubia na Jumuiya hiyo.

“Wahusika walishakuja mbele ya kikao cha kamati ya utekelezaji na tukashauriana kukutana na wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Wazazi kwa uamuzi wa mwisho.

“Uamuzi ukifikiwa nitakuwa tayari kusimamia uanzishwaji wake kwa kuwa naona jambo hili ni jema kwa Jumuiya yetu, ikizingatiwa UWT na UVCCM wana benki inayofanya kazi na nyingine iko mbioni kuanzishwa,” alisema Bwanamdogo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa