Home » » TUGHE YAWASHUKIA WAKURUGENZI

TUGHE YAWASHUKIA WAKURUGENZI

na Julieth Mkireri, Kibaha
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Ally Kiwenge, ameeleza kusikitishwa na kitendo cha baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri kuwahamisha viongozi wa matawi wa chama hicho, baada ya kuibua ubadhirifu unaofanyika katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kiwenge alisema wakati serikali inalia na ubadhirifu wa mali, wapo wanaowakumbatia watendaji wasio waadilifu na kusababisha wananchi waendelee kuilalamikia.
Kimwenge alisema chama hicho hakina ugomvi na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na hakiko tayari kuibua migogoro na serikali, hivyo ni vema wakurugenzi wakasimamia vizuri maagizo ya serikali badala ya kuendelea na tabia ya kuwahamisha wanachama wa chama hicho wanaosimama kutetea wafanyakazi wenzao na kusimamia matumizi mabaya ya rasilimali za umma.
Katibu huyo alisema hivi karibuni baada ya Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia kutembelea Mkoa wa Geita na kuzungumza na wafanyakazi, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Geita, Mary Muntu aliibua kero mbalimbali wanazopata wafanyakazi, jambo ambalo waziri huyo aliahidi kuzifanyia kazi.
Hata hivyo, Kiwenge alieleza kuwa katika hali ya kushangaza mwenyekiti huyo amehamishiwa katika kituo cha afya cha Kikobe umbali wa kilometa 80 kutoka Geita, hivyo atashindwa kushughulikia matatizo ya wanachama wake.
Kutokana na hali hiyo, alisema chama hicho kinatarajia kuanza kukusanya taarifa mbalimbali juu ya uhamisho wa mwenyekiti wao na wakikamilisha watawaburuza wahusika mahakamani.
Chanzo: Tanzania Diama

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa