Home » » CCM WAASWA KUCHAGUA VIONGOZI BORA

CCM WAASWA KUCHAGUA VIONGOZI BORA

na Julieth Mkireri, Kisarawe
BAADHI ya viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, wameaswa kuachana na tabia ya kupanga safu kabla ya chaguzi kufanyika, kwani kufanya hivyo kunachangia kupatikana kwa viongozi wasio na sifa.
Rai hiyo ilitolewa mjini hapa na Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo, wakati akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM.
Kwa mujibu wa Jafo, changamoto kubwa iliyopo ndani ya chama hicho ni kujipanga kwa kujigawa makundi, nongwa zisizoisha nyakati za chaguzi, hali inayosababisha kukishushia sifa chama hicho.
“Muda mwingi jamani utumike kutatua matatizo ya wananchi na kutekeleza miradi inayoibuliwa na wanajamii, ili chama kisonge mbele kuliko kutumia muda mwingi kusemana na kusengenyana kwa mambo yasiyo na msingi,” alisema Jafo.
Alitumia nafasi hiyo kuahidi kutimiza vipaumbele alivyoahidi kwa wananchi wa jimbo lake na kuahidi kuendelea kuwa nyuma ya wananchi wake kwa miaka mitatu ya uongozi wake iliyobaki.
Aliwaomba vijana kuunda vikundi vitakavyosaidia kupatiwa misaada kirahisi kutoka kwa wafadhili wanaojitokeza badala ya kujiweka mmoja mmoja hususan katika shughuli za kijasiriamali.
Katika hatua nyingine, Chama cha Mapinduzi wilayani humo mwishoni mwa wiki  kimefanya mapokezi makubwa  kwa mbunge huyo kwa lengo la kumpongeza kwa kutoa hoja binafsi bungeni ambayo inalenga kuwatetea wafanyakazi nchini kupata mafao yao muda wowote mara baada ya kuacha kazi ama kustaafu.
Uongozi wa chama hicho uliandaa mapokezi hayo makubwa wakilenga kumpongeza Jafo pamoja na kumpa motisha ya kutoa hoja nyingine  za kutetea wananchi wa jimbo hilo na Tanzania kwa ujumla pindi awapo bungeni.
Akiwashukuru wanachama hao, Jafo alisema kuwa kabla ya kufikisha hoja hiyo bungeni alitafakari maisha ya Watanzania ambao wengi wao itakuwa vigumu kusubiri hadi baada ya miaka 55 hadi 60 ndipo wapate mafao yao, jambo ambalo ni kugumu kutafakari na kulitekeleza.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa