Home » » AMUUA MAMA YAKE MZAZI KWA JEMBE

AMUUA MAMA YAKE MZAZI KWA JEMBE

Na Gustaphu Haule, Bagamoyo
JESHI la Polisi Mkoani Pwani, linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Mwidu, kilichopo wilayani Bagamoyo, Juma Shaban (29), kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi kikatili.

Shabani anadaiwa kumuua mama yake, Zena Rajabu (59) mkazi wa kijiji hicho, kwa kumkatakata na jembe na kisha kuutenganisha mwili wake katika mafungu mbalimbali yasiyobebeka.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akiwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea jana asubuhi kijijini humo.

Mangu alisema baada ya kitendo hicho, hatua iliyofuata alianza kutenganisha mwili wa mama yake katika mafungu mbalimbali, ikiwemo mikono, miguu, kiwiliwili pamoja na utumbo.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea  wakati mama mzazi wa kijana huyo akiwa shambani akichimba mihogo, ndipo alipotokea kijana huyo na kuanza kumshambulia mama yake kwa kutumia jembe na kisha kumsababishia kifo.
Hata hivyo sababu za kufanya hivyo hazikuweza kufahamika. "Kitendo alichofanya kijana huyo ni cha ukatili, kwani baada ya kumuua alianza kutenganisha mwili wa mama yake katika mafungu mbalimbali,” alisema.

Mangu aliongeza kuwa wakati kijana huyo akifanya unyama huo, baadhi ya wananchi walisikia mama huyo akipiga kelele na kuamua kwenda katika eneo la tukio, lakini kutokana na umbali walifika na kukuta tayari mama huyo amefanyiwa unyama huo.

Aidha wananchi waliofika katika eneo hilo walimkuta kijana huyo na kuanza kumvamia kwa kutaka naye auawe kama alivyomuua mama yake mzazi, lakini walifanikiwa kumjeruhi kijana huyo na kumvunja mguu mmoja.

Kutokana na mwili wa marehemu Zena kuharibiwa vibaya, haikuwezekana kubebwa na badala yake ulizikwa katika eneo la tukio, huku kijana huyo akiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha chini ya uangalizi wa Polisi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa