HALI ya usalama mkoani Pwani imeimarika kwa asilimia 99 kutokana na
Polisi kudhibiti uhalifu. Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jonathan Mshana
alisema jana kuwa hivi sasa vyombo vya dola vinaendelea kusaka mabaki
ya wahalifu hao kila kona nchini ili wawachukulie hatua za sheria.
“Naweza kusema uhalifu umekwisha na kufikia pointi sifuri.
Tunaendelea kuvisaka vimelea vidogo vidogo vya wahalifu hao nyumba kwa
nyumba popote walipo tutawapata,” alisema Kamanda Mshana.
Pasipo kutaja takwimu, Kamanda Mshana alisema matukio hayo ya uhalifu
Pwani yaligharimu maisha ya viongozi na watendaji wa vijiji pamoja na
askari lakini pia wahalifu nao walipoteza maisha.
Kutokana na watendaji wa vijiji kupoteza maisha na wengine sifa ya
kuwa viongozi, Halmashauri za Wilaya ya Mkuranga na Kibiti zilitangaza
nafasi za kazi kuziba nafasi hizo za watendaji zilizokuwa wazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mshamu
Munde alisema nafasi 66 za watendaji wa kijiji zilizotangazwa Agosti
mwaka huu zitazibwa rasmi wiki hii na watendaji wapya.
Munde alisema walipokea maombi zaidi ya 1,500 ya watu walioomba
nafasi za watendaji wa kijiji. Alisema baada ya usaili, wiki hii
watawaajiri waende wakaanze kazi katika vijiji watakavyopangiwa.
“Ajira hii ni ya kuziba nafasi za watendaji wa awali ambao wengi
walipoteza sifa ya kuendelea kuwa watendaji wa vijiji kama kukosa elimu
ya kidato cha nne, kuziba nafasi za watendaji waliopoteza maisha
kutokana na mauaji,” alieleza Munde.
Alisema kupitia uhakiki wa watumishi wa umma, ilibainika watendaji 66
hawakuwa na sifa kwa kukosa elimu ya kidato cha nne na kupoteza ajira
zao. Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Alvera
Ndabagoye alisema nafasi 45 za watendaji wa kijiji zilizotangazwa Agosti
mwaka huu zimeshapata watu wa kuziziba.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment