Home » » TEKNOLOJIA KUDHIBITI AJALI BARABARANI YAJA

TEKNOLOJIA KUDHIBITI AJALI BARABARANI YAJA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


MAENEO yenye ajali zaidi nchini, ukiwamo Mkoa wa Pwani, yatafungwa rada, ili kupata taarifa zaidi na chombo kilichohusika na kusababisha ajali.

Aidha, mkoa huo umefanikiwa kupunguza matukio ya ajali kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2016 kutoka ajali 306 hadi 58 mwaka huu katika kipindi kama hicho.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Jonathan Shanna, aliyasema hayo jana, wakati akifungua semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari namna ya kuripoti kwa usahihi ajali na elimu kwa umma kuhusu sheria za barabarani yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa).

Alieleza ajali nyingi zinatokana na makosa na ukiukwaji wa sheria za barabarani ikiwamo spidi kubwa, ulevi na kutotumiwa vikinga mwili kabla ya ajali kama kofia ngumu kwa bodaboda na mikanda kwenye magari.

Alisema katika kipindi kama hicho, vifo vilivyotokana na ajali mwaka 2016 vilikuwa 118 na vimeshuka hadi 49 huku ajali zinazoongoza zikiwa ni za bodaboda.

Alisema waendesha bodaboda wengi hawana elimu ya usalama barabarani, wana umri mdogo, hawana leseni licha ya sheria kueleza dereva anayetakiwa kupatiwa leseni ni mwenye zaidi ya miaka 18.

“Mkakati ni kuhakikisha ajali zinapungua kabisa kwa kuhakikisha doria inaimarishwa, kukagua magari ya masafa marefu, kupima kiwango cha vilevi kwa madereva na kutoa mafunzo zaidi kwa watumia barabara,” alisema Shanna.
Alisema madereva ambao waendesha kwa spidi kubwa wataendelea kupigwa faini kulingana na sheria za usalama barabarani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani huko, Abdi Isango, alisema kati ya maeneo ambayo yalifanyiwa utafiti kutokana na ajali za barabarani mkoani humo, ni eneo la Ruvu.

“Wataalamu walifika kubaini kati ya maeneo yenye ajali zaidi mojawapo ni Ruvu, na utafiti huu unakwenda barabara kuu hadi mkoani Mwanza, ili zifungwe rada ambazo zitatupa taarifa na kupata kumbukumbu,” alisema Kamanda Isango.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa