Frank Mvungi-Maelezo
Serikali imesema kuwa
inaridhishwa na hali ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa mtambo
wa maji Chalinze na ujenzi wa mfumo wa kusafirishia na kusambaza maji pamoja na
matenki ya kuhifadhi maji utakaozalisha zaidi lita milioni tisa
utakapokamilika.
Akizungumza wakati wa
ziara yake ya kukagua mradi huo
utakaonufaisha wakazi zaidi ya laki tatu wa Jimbo la Chalinze na Wilaya
ya Handeni Mkoa wa Tanga, Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji
Mhandisi Ezekiel Kamwele amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuona
wananchi wanapata huduma ya maji kwa wakati kupitia maradi huo unaotarajiwa
kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu.
“Mradi wa Lindi
umekamilika na hapa lazima tuchukue hatua kama Lindi ili kutatua changamoto
zinazoweza kukwamisha kukamilika kwa mradi kwa wakati na kwa kuwa wametupa mpango kazi wao
tunaamini kazi itakamilika kwa wakati na nitafuatilia kila hatua “ Alisisitiza
Mhandisi Kamwele.
Akifafanua Mhandisi
Kamwele amesema kuwa katika kila eneo la mradi alilokagua ikiwemo ulazaji wa
mabomba, ujenzi wa matenki ya kusambazia maji ameridhishwa na kasi ya utendaji
na kuipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASA) kwa
usimamizi mzuri katika utekelezaji wa miradi ya maji wanayokabidhiwa.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze
(CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchomba amesema kukamilika kwa mradi huo
kutasaidia kukuza shughuli za kiuchumi zikiwemo za viwanda kwa kuwa tayari
wamepokea maombi ya Viwanda kadhaa kuunganishwa katika mtandao wa maji,viwanda
hivyo ni Kiwanda cha shurubati (juisi), Kiwanda cha kutibu mbao, pamoja na Kiwanda
cha kuzalisha vigae .
Aliongeza kuwa mradi
huo pia utasidia kuinua shughuli za Kilimo na ufugaji hali itakayosaidia kukua
kwa sekta ya Viwanda hali itakayochochea kukua kwa uchumi.
“Awamu ya Tatu ya mradi huu inagharimu bilioni 84 hadi
kukamilika kwake na huu ni mradi mkubwa utakaowanufaisha wananchi wengi” Alisisitiza
Mhandisi Mchomba.
Katika kutekeleza
mradi huo ulazaji wa mabomba ya
kusafirishia maji umefikia km 96.8 kati ya
km 115 na ujenzi wa ofisi umefikia asilimia 82.
Kwa upande wake
Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Rupungwi Chalinze ambacho ni sehemu ya vijiji
vinavyonufaika na mradi huo amesema wananchi wanapongeza Serikali kwa kuwaletea
mradi huo utakaoinua shughuli za kiuchumi.
Mradi huu
unatekelezwa kupitia mkopo kutoka India na mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe
18 Mei, 2015 kati ya DAWASA na Kampuni ya Overseas Infrastracture Pvt Ltd
ikishirikiana na PIL zote za India.
0 comments:
Post a Comment