Imeandikwa na John Gagarini, Kibaha
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amekubali maombi ya Kituo cha Afya cha Mlandizi kuwa Hospitali
ya wilaya.
Alitoa tamko hilo kwenye uwanja wa Mtaongani Mlandizi wilayani Kibaha
wakati akipokea magari mawili ya kubeba wagonjwa na vitanda vitatu vya
kuzalishia wajawazito kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini,
Hamoud Jumaa na gari moja kutoka kwa Rais John Magufuli.
Alisema ombi lililotolewa na mbunge huyo kwa viongozi wa ngazi za juu
na kwake amelikubali, hivyo Mganga mkuu wa wilaya anapaswa kuandika
barua na kuzipeleka sehemu husika kisha zifikishwe wizarani kwa ajili ya
utekelezaji.
“Mbunge wenu amekuwa akipigania kituo hiki kwa muda mrefu kama
alivyosema, hivyo naona hakuna kipingamizi ili mradi tu taratibu
zifuatwe kufikia hatua hiyo, lengo kubwa ni kuboresha huduma kwa
wananchi,” alisema.
Awali Jumaa alisema maombi hayo alishayatoa kwa viongozi mbalimbali
ikiwemo kwa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli.
Jumaa alisema kuwa kituo hicho kwa sasa kinahudumia watu wengi tofauti
na ilivyokuwa zamani ambapo kwa sasa wanakaribia watu 100,000, hivyo
kuna haja kabisa ya kuwa hospitali ya wilaya.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment