Waliouawa wawili, yapora bunduki saba na risasi kibao, Ni tukio la tatu katika miezi saba, IGP atangaza bingo ya milioni 20/-
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
Katika kipindi cha miezi saba sasa kuanzia Juni, mwaka jana hadi
Januari, mwaka huu, vituo vya polisi vitatu vimetekwa, askari polisi
watano na mgambo mmoja wameuawa na silaha za aina mbalimbali takribani
20 zimeporwa katika vituo vilivyovamiwa.
Uvamizi wa vituo hivyo ulianza katika kituo kidogo cha polisi
Mkamba kilichopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani baadaye kituo cha
polisi Bukombe kilichopo mkoani Geita na sasa kituo cha polisi Ikwiriri
wilayani Rufiji, mkoani Pwani.
Katika tukio lililotokea usiku wa kuamkia jana, watu 10
wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za jadi na za moto
walikiteka kituo cha polisi Ikwiriri kilichopo Tarafa ya Ikwiriri
wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kuwaua askari wawili, kupora silaha
saba kisha kulipua bomu kituoni hapo.
MAELEZO YA RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, akizungumza na
NIPASHE jana, alisema tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku wa kuamkia
jana.
Kamanda Matei alitaja askari waliouawa katika tukio hilo kuwa ni
askari mwenye namba WP 5558 PC Judith Timoth na E.8732 Koplo Edga Mlinga
ambaye ni askari wa kikosi cha usalama barabarani na kwamba miili ya
askari imehifadhiwa katika kituo cha afya Ikwiriri.
Alisema katika tukio hilo majambazi hao ambao idadi yao
haijajulikana, baada ya kukivamia kituo hicho walifanikiwa kuiba bunduki
aina ya SMG mbili, SAR mbili, shotgun moja, risasi zaidi ya 60 na
bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
Kamanda Matei ambaye alikuwa akizungumza akiwa eneo la tukio,
alisema baada ya kufanya unyama huo majambazi hao walilipua bomu kituoni
hapo ambalo liliharibu gari lenye namba PT 1965 linalotumiwa na Mkuu wa
Upelelezi wa Kituo hicho (OCCID) kisha kutokomea kusikojulikana.
Alisema kufuatia tukio hilo msako mkali wa kuwabaini watu
waliohusika na tukio hilo unafanyika ingawa hadi jana mchana, hakuna mtu
aliyekuwa akishikiliwa kuhusika na tukio hilo.
KAULI YA DC
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu, alisema
majambazi hao ambao wanasadakiwa kuwa 10 walikivamia kituo hicho cha
polisi wakiwa na mapanga, visu na silaha za moto, ambazo hata hivyo
hakuzitaja.
Alisema walipofika kituo hapo walipiga risasi mfululizo hewani na
baadaye wakaingia ndani ya kituo na kuanza kuwacharanga kwa mapanga na
visu askari hao hadi wakafariki.
Babu alisema baada ya kufanya mauaji hayo waliingia katika chumba zilimokuwamo silaha na kuziba zote.
Babu alisema baadaye walipiga risasi nyingine hewani ili kuwatisha
wananchi wasiweze kusogea kituo kisha walitupa bomu ambalo liliharibu
gari la OCCID.
Alisema bomu hilo lililorushwa na majambazi hao liliharibu kioo cha
gari la OCCID upande wa kushoto na pia walipiga risasi matairi yote ya
gari hilo.
IGP ATUMA MAKACHERO
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu,
amemtuma Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Paulo Chagonja
pamoja na makachero kadhaa kwenda wilayani Rufiji kuchunguza kwa undani
tukio hilo na kuwasaka wahusika.
“IGP Mangu ameshatoa agizo na hivi sasa unavyoongea na mimi
Kamishna Chagonja na makachero kadhaa wapo njiani wanakwenda Rufiji,”
alisema Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Diwani
Athumani.
CHAGONJA ANENA
Naye Kamishna Chagonja akizungumza na gazeti hili akiwa Rufiji,
alisema hadi kufika jana jioni hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa kuhusiana
na tukio hilo na kwamba msako bado unaendelea.
Taarifa zaidi ambazo gazeti hili ilizipata kutoka eneo la tukio
zinaeleza kuwa majambazi hao pia walizitoa upepo pikipiki zote
zilizokuwapo kituoni hapo ili kuzuia wasifuatiliwe.
Taarifa zikizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zinaeleza kuwa
miili ya askari waliouawa ilipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Mkuranga na maofisa wa polisi walikuwa wakiendelea na kikao kujadili
suala hilo.
IGP ATANGAZA BINGO YA MILIONI 20/-
Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP Advera Bulimba, alisema kufuatia
tukio hilo, IGP Mangu ametenga Sh. milioni 20 ambazo zitatolewa kama
zawadi kwa mtu ambaye atatoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watu
waliofanya tukio hilo.
Kamanda Bulimba alisema wananchi wasiwe na wasiwasi kwani jeshi
hilo bado lipo imara na kuwataka watoe ushirikiano kwa polisi ili
kufanikisha kuwakamatwa kwa waliohusika katika tukio hilo.
“IGP Mangu amelaani vikali tukio hilo ambalo ni sawa na la kigaidi
ambalo halikubaliki duniani kote, tutahakikisha tunawasaka na kuwatia
mbaroni wahusika wote walioua polisi wetu na kupora silaha,” alisema
Bulimba akimnukuu IGP.
MATUKIO YA MAUAJI YA POLISI
Hili ni tukio la pili kuvamiwa kituo cha polisi katika mkoa wa Pwani na kusababisha mauaji.
Tukio la kwanza lilitokea Juni 11, mwaka jana baada ya watu
wasiojulikana walipokivamia kituo kidogo cha polisi Mkamba na
kusababisha kifo cha askari mmoja na mgambo.
Askari aliyefariki ni mwenye namba D 9889 koplo Joseph Ngonyani
ambaye alifia katika Hospitali ya wilaya ya Mkuranga wakati akitibiwa
kutokana na kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
Katika tukio hilo, mgambo, Venance Francis, naye alifariki wakati
akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wakati askari
Mariamu Mkamba aliyejeruhiwa alipatiwa matibabu na kupona.
Majambazi hayo katika tukio hilo walipora bunduki aina ya Shortugun
tatu, SMG mbili na magazine 30 kila moja ambazo zilikuwa kwenye ghala
la muda zikisubili kupelekwa kwenye kituo kikubwa kwenye ghala kuu la
silaha.
Tukio jingine la kuvamiwa kituo cha polisi lilitokea Septemba mwaka
jana katika kituo kikuu cha polisi wilayani Bukombe mkoani Geita ambako
askari wawili waliuawa na kujeruhi wengine watatu. na bunduki 10
kuporwa.
Mbali na kupora SMG 10, pia inadaiwa walifanikiwa kupora risasi
ambazo idadi yake haikutambulika mara moja pamoja na mabomu ya kutupa
kwa mkono na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo, aliwataja askari
waliouawa kuwa ni WP 7106 Uria Mwandiga na G. 2615 PC Dustani Kimati na
waliojeruhiwa askari namba E.5831 CPL David Ngupama Mwalugelwa
aliyejeruhiwa kichwa na usoni huku akiumizwa mdomo na meno mawili
kungooka pamoja na Mohamed Hassan Kilomo ambaye alijeruhiwa kwa risasi
kifuani na mguu wa kulia kwa.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment