Home » » WAWEKEZAJI WADAIWA KUCHAFUA MAZINGIRA NA AFYA ZA WATU

WAWEKEZAJI WADAIWA KUCHAFUA MAZINGIRA NA AFYA ZA WATU

Wawekezaji wa China wanaotafuta madini wilayani Mkuranga mkoani Pwani, wanadaiwa kuchafua mazingira na kutishia afya za watu na mifugo yao.
 
Kufuatia hatua hiyo Kamati ya Huduma za Uchumi na Mazingira  imetoa wiki mbili kwa viongozi wa  Mkuranga, kuwaleta wataalamu wa mazingira  na kupata maoni yao kuhusu hatma ya afya za wananchi.
 
Waliagiza watendaji hao kuwasiliana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufika katika kata ya  Shungubweni ili kuchunguza maji hayo.
 
"Tunaomba wakuu wa idara ya mazingira wawalete wataalamu kutoka (NEMC) kuyakagua maji hayo, kama watashindwa kuwaleta sisi viongozi tutachukuwa jukumu la kuwafukuza Wachina hao,''ilisema.
 
Wachina wanadaiwa kumwaga  taka ndani ya  vyanzo vya maji na kuchafua maji hayo ambayo sasa ni ya njano na yanapomwagiliwa mimea  hukauka.
 
Taarifa ya kamati ambayo NIPASHE ina nakala yake ilisema madini yanayochimbwa ni ‘silicon na titanium’ na kwamba tangu uchumbaji huo uanze wananchi hawajanufaika.
 
Iliongeza kuwa, kutokana na wawekezaji  hao kuchimba madini na  kutupa uchafu katika vyanzo vya maji wanakijiji wanahofu kwani maji yamebadilika rangi  licha ya kwamba wanaendelea kuyatumia pia kunywesha mifugo  yao.
 
Uchimbaji huo umeanza mwaka juzi na hawajawahi kunufaika na kwamba  halmashauri haijaona maendeleo ya uwekezaji huo.
Diwani wa Kata ya Shungubweni Nassoro Kirapo, alisema  Wachina hao walifika katika kijiji chao na kuwalipa fidia wanakijiji kuendana na maeneo yao ili waweze kuchimba mchanga kwa ajili ya kutafuta madini.
 
Alisema pia kuwa waliahidi baada ya kuyachukuwa maeneo hayo watawawasaidia  kuboresha miundombinu na  maendeleo.
 
"Toka waanze kuchimba mwaka juzi mpaka sasa hakuna hata siku moja wealiowahi kuwasaidia wanakijiji katika kuboresha maeneo yao, ila wamenchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu miundombinu,''alisema.
 
 
''Kutokana na kamati kuona mazingira yalivyoharibiwa wajumbe wameamua kutoa wiki mbili kwa wakuu wa idara ya mazingira kuwasiliana na NEMC ili kuchunguza maji kama yatakuwa na madhara kwa binadamu na mifugo  ili hatua zichukuliwe mapema,''alisema.
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. KUELEKEA UCHAGUZI 2015: JE UNAPENDA NANI AWE KIONGOZI WAKO? JAZA FOMU HII FUPI HAPA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa