CHAMA cha Walimu (CWT) Mkoa wa Pwani, kimetoa agizo kwa Halmashauri
za Wilaya za Kibaha, Kisarawe na Bagamoyo kuharakisha malipo ya walimu
ya zaidi ya sh 16,450,000, ili kuepusha mgomo.
Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Pwani, Kelvin Mahundi, alitoa tamko hilo juzi alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mgomo walimu wa mkoa huo.
Alisema pamoja na serikali kutuma fedha za walimu waliohakikiwa kuna walimu wengi wa mkoa huo ambao wanaidai serikali hawajakamilishiwa fedha zao na halmashauri, jambo ambalo linaweza likasababisha mgogoro kati ya chama hicho na halmashauri.
Mwenyekiti huyo alisema walimu hao ni wale waliopo chini ya Katibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; na walimu waliopo kwenye halmashauri ambao mafaili yao hayakufikishwa kwenye uhakiki kutokana na muda kuwa mdogo na uzembe wa watendaji wa halmashauri husika.
Aidha, aliongeza kuwa walimu hao zaidi ya 170 ni wale walioanza kazi mwaka 2003 katika wilaya za Kisarawe, Kibaha na Bagamoyo ambapo wanadai posho ya kujikimu ya sh 7,350,000 na walimu walioanza kazi mwaka 2005 katika wilaya za Kibaha na Kisarawe ambao pia ni zaidi ya 65 na wanadai ya sh 9,100,000.
Aliwaomba Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo waliopewa dhamana ya kusimamia uhakiki mpya kuharakisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya za Kibaha, Kisarawe na Bagamoyo kutoa maelezo ya kushindwa kutoa posho ya kujikimu kwa walimu walioanza kazi mwaka 2003 na 2005 na kueleza matumizi ya fedha hizo.
"Wakurugenzi wa Halmashauri hizi ambazo hazijakamilisha malipo kwa walimu wanatakiwa kujieleza kwa nini walishindwa kuwalipa walimu posho ya kujikimu kwa mwaka 2003 na 2005 huku Halmashauri nyingine zikiweza kutekeleza malipo hayo, wao fedha hizi walizipeleka wapi?” alihoji mwenyekiti huo.
Mahundi pia aliishauri serikali ya mkoa huo kuandaa bajeti ya kutosha kwa kila mwaka, ili walimu walipwe kwa wakati na si kulundika madeni
Chanzo;Tanzania
Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment