Home » » MSALABA MWEKUNDU MAILIMOJA WAPIGWA TAFU

MSALABA MWEKUNDU MAILIMOJA WAPIGWA TAFU

CHAMA cha Msalaba Mwekundu tawi la Mailimoja Kibaha mkoani Pwani, kimepokea dawa, vifaa pamoja na fedha kutoka kwa mke wa mbunge wa Kibaha mjini, Selina Koka ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Msaada huo umekabidhiwa mjini hapa juzi kwa Mwenyekiti wa chama hicho tawi la Mailimoja, Lazaro Kuligwa, muda mfupi baada ya uzinduzi wa klabu ya Makaparo iliyo chini ya chama hicho.
Msaada huo wa vifaa vyenye thamani ya sh 500,000 pamoja na fedha taslim sh milioni moja vitasaidia chama hicho kufanya kazi zake kwa ufanisi kutokana na hapo awali kukabiliwa na changamoto ya vifaa iliyokuwa inasababisha kufanya kazi zao chini ya kiwango.
Selina, alisema Chama cha Msalaba Mwekundu ni muhimu kwa jamii, kwani kinasaidia kutoa huduma ya kwanza kabla mgonjwa kufikishwa hospitali, hivyo ni vema kukawa na vifaa vya kutosha kufanya kazi zao kwa kiwango kinachotakiwa.
Aidha, aliwasasihi wanawake kujitokeza kwa wingi kujiunga na chama hicho, badala ya kuachia nafasi kubwa kwa wanaume.
Kwa upande wake, Kuliga alisema chama chao ambacho kina wanachama 280 kwa sasa, kinawahudumia wazee tisa wenye miaka 60 kupatiwa matibabu na mahitaji mengine.
Kuliga, alisema changamoto kubwa inayokabili chama hicho ni pamoja na suala zima la ajira, hasa ukizingatia chama hicho kazi zake nyingi ni zakujitolea na hivyo wanachama kulazimika kuchangishana pale inapohitajika kufanya kazi za chama.
Alimuomba mke wa mbunge huyo aliyeridhia kuwa mlezi wa chama hicho, kushirikiana nao bega kwa bega kutatua changamoto za chama hicho ili kiendelee kufanya kazi zake katika maeneo mengi ya mji huo.
 Chanzo;Tanzania daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa