Home » » MAAMBUKIZI YA VVU PWANI YASHUKA

MAAMBUKIZI YA VVU PWANI YASHUKA

HALMASHAURI ya Mji Kibaha mkoani Pwani jana imefanya Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi huku tathmini ya jumla ikionesha kushuka kwa maambukizi mapya ikilinganishwa na tathmini ya mwaka jana.
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Siwema Cheru alitoa takwimu hizo alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kudhibiti ugonjwa huo kwa mgeni rasmi, Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka.
Cheru alisema Halmashauri ya Mji Kibaha imeweka mipango na mikakati ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU na Ukimwi kwa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuendelea kupata ushauri na kupima ambapo wanaogundulika kuwa na maambukizi huanzishiwa dawa za kufubaza makali.
Aidha Cheru alisema kutokana na waraka uliotolewa na Serikali juu ya kudhibiti maambukizi mahala pa kazi, ofisi yake imetoa Sh milioni tatu kusaidia watumishi 10 wanaoishi na maradhi hayo kununulia lishe pamoja na dawa kwa lengo la kuboresha afya zao. Cheru alisema kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu watu 11,996 wamejitokeza kupima afya zao.
Wanawake ni 6,806 na wanaume 5,190. Kati ya hao, 1,064 sawa na asilimia 8.7 walipatikana na maambukizi mapya. “Maambukizi haya yamepungua kwa asilimia moja kwani mwaka 2013 Halmashauri ya Mji Kibaha ilikuwa na asilimia 9.7,” alisema.
Kwa upande wake, Mbunge Koka alitaka wananchi kubadili tabia kunusuru taifa. “Ninafahamu, sote tunafahamu njia ambazo gonjwa hili linavyoambukizwa, hatuna budi kupigana vita kwani litatumaliza,” alisisitiza.
Mbunge huyo alikemea Watanzania kutegemea misaada ya wahisani kutoka Ulaya kutokomeza Ukimwi na kusema kuwa iwapo kila mwananchi kwa nafasi yake atabadili tabia, Tanzania bila ugonjwa huo inawezekana.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa