KATIBU Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya
(Tughe), John Sanjo, ameutaka uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
jijini Dar es Salaam, kuhakikisha wanatatua haraka changamoto na kesi
zinazojitokeza baina ya wanachama wake na uongozi.
Sanjo, alitoa rai hiyo Mjini Kibaha juzi wakati akizungumza na
Waandishi wa Habari kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazowakabili
wafanyakazi wa Muhimbili ambao pia ni wanachama wa Tughe.
Kauli ya Sanjo, imekuja baada ya kupata malalamiko kutoka kwa baadhi
ya wafanyakazi wa hospitalini hiyo, ambako alibainisha kama kesi hizo
zitakuwa zinalimbikizwa bila kutatuliwa ni wazi watasababisha wataalamu
waliopo Muhimbili kukata tamaa ya kufanya kazi.
Sanjo, alisema moja ya changamoto hizo ni pamoja na wauguzi kukosa
fedha za kununulia sare, ambako kwa mujibu wa utaratibu kila muuguzi
anapaswa kupewa sh 300,000 badala ya 120,000.
“Kwa kweli wafanyakazi wa Muhimbili wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo ya kukosa fedha za likizo, kushindwa kupata
fedha za kiinua mgongo, sare kwa wauguzi na hata kantini ya chakula,
hali ambayo inaathiri utendaji kazi kwa watumishi hao,” alisema Sanjo.
Alisema Tughe itaendelea kupigania maslahi ya wanachama wake kwa
kukaa meza moja na uongozi wa Muhimbili, ili kuona jinsi ya kutatua
changamoto hizo lakini pia amewataka kuwa wavumilivu wakati changamoto
hizo zikifanyiwa kazi.
Hata hivyo, alisema ili kukomesha changamoto hizo ni vyema pia
serikali ikaweka Mkurugenzi Mtendaji ambaye anatokana na wafanyakazi
wenyewe, kwani atakuwa anatambua changamoto zilizopo na namna ya
kuwasaidia wenzake kuliko kila mwaka kumtoa Mkurugenzi Muhas.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment