BAADHI ya halmashauri za wilaya za mkoani Pwani ambazo hazina hata kilometa moja ya barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami zimetakiwa kuwa na ubunifu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kujenga barabara hizo badala ya kusubiri Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Ushauri huo ulitolewa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza, wakati wa Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo.
Mahiza alisema kuwa inashangaza kuona hakuna jitihada zozote zikifanyika za kuhakikisha kunakuwa na ujenzi wa barabara za lami.
“Kaeni na wadau wenu, jengeni barabara za lami hata kilomita moja moja mfano mzuri ni Halmashauri ya Mji wa Kibaha imejenga lami kidogo kidogo kwenye baadhi ya maeneo lakini halmashauri zingine hazifanyi jitihada kama hizo,” alisema Mahiza.
Aidha alisema kama halmashauri hazina uwezo zinaweza kuingia mikataba na wajenzi wa barabara ili baadaye wawalipe.
“Mji wa Kibaha ulikopa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zake kwa kiwango cha lami kwa hiyo na halmashauri nyingine ziige mfano huu kwani kikubwa ni ubunifu msikubali kukaa tu,” alisema Mahiza.
Alibainisha kuwa kuna halmashauri zina vyanzo vingi vya mapato ambavyo vinaweza kuwasaidia katika kufanikisha ujenzi huo kwani haipendezi kutokuwa na lami ambayo inapendeza na inapunguza ukarabati wa mara kwa mara unaotumia fedha nyingi.
Naye, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Mhandisi Tumaini Sarakikya alisema uwezo wao si mkubwa kutokana na kutokuwa na fedha nyingi kwani wanategemea kutoka serikalini.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chanzo;Habari Leo
0 comments:
Post a Comment