Waatalamu wa Sekta za Nishati na Madini, wametakiwa kuwa wabunifu katika maandalizi na usimamizi wa miradi ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Wito huo ulitolewa na Kamishna msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, alipokuwa akifungua mafunzo ya uandaaji wa mapendekezo ya miradi, sera na mbinu za usimamizi wa miradi, yaliyoshirikisha wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TDGC) yanayoendelea mjini Bagamoyo.
Mafunzo haya yanatolewa na mtaalamu mwelekezi ambaye ni kampuni ya Petrogas yenye makazi yake jijini Dar es Salaam, ambapo kwa niaba ya kwa niaba ya Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Hosea Mbise, Mhandisi Luoga alisema kuwa Serikali imekuwa ikikumbana na changamoto mbalimbali katika usimamizi wa miradi yake ya maendeleo.
Alisema ni vyema wataalamu hao mara baada ya kumaliza mafunzo hayo wakawa wabunifu kiasi cha kuweza kuandaa mapendekezo ya miradi yanayotekelezeka, huku yakiendana na kiasi cha bajeti iliyotengwa.
“ Kama Wizara tuna kazi nyingi zinazotakiwa kutekelezwa ambazo zinahitaji uandaaji makini wa mapendezo ya miradi ambazo zinahitaji utaalamu wa hali ya juu kuanzia uanzilishi wa miradi, utekelezaji wake na tathmini yake kulingana na kiasi cha fedha kilichotengwa,”alisema Luoga.
Naye msimamizi wa mradi unaohusika na kuwajengea uwezo wataalamu wa nishati na tasnia ya uziduaji, Paul Kiwele alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wataalamu kutoka sekta za nishati na madini katika uandaaji wa mapendekezo ya miradi mbalimbali na sera ili kuepusha gharama ya kutumia wataalamu kutoka nje na kukuza umiliki.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment