Home » » JAFO ATOA MILIONI 71 KUKAMILISHA MIRADI YA MAENDELEO

JAFO ATOA MILIONI 71 KUKAMILISHA MIRADI YA MAENDELEO

MBUNGE wa Kisarawe, mkoani Pwani, Selemani Jafo (CCM) ametoa shilingi milioni 71 kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya miradi ya maendeleo jimboni humo ikiwemo ujenzi wa maabara unaoendelea katika shule za sekondari.
Akizungumzia kuhusiana na miradi inayotekelezwa kwa fedha hizo, Jafo alisema milioni 40 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Ving’andi kata ya Mafizi tarafa ya Mzenga.
Jafo alibainisha kuwa milioni 20 zitatumika kufungua barabara ya Dololo inayokwenda kijiji cha Ving’andi na milioni 11 kwa ajili ya ununuzi wa mabati 600 yatakayogawanywa kwenye shule za sekondari sita ili kukamilisha ujenzi wa maabara unaoendelea.
Aidha mbunge huyo alisema kijiji cha Ving’andi kilisahaulika kupatiwa huduma za kijamii kwani kilikuwa hakina zahanati ya kukiunganisha na vijiji vingine tangu kianzishwe.
Jafo alisema, wakazi wa kijiji hicho walikuwa wakitembea urefu wa km 28 kufuata huduma za afya eneo la Gwata jambo ambalo lilikua linaleta usumbufu mkubwa hasa kwa akina mama wajawazito na watoto waliokua wakihitaji huduma ya kupelekwa kliniki.
“Nilivyoingia madarakani niliiona hali hii ambayo ilikua inaniumiza kama mzazi, katika kutafakari hili ilinilazimu kutenga fedha kutoka kwenye mfuko wa jimbo kusaidia kutatua changamoto katika kijiji hiki na sasa nayaona mafanikio, nawaomba wananchi tuendelee kushirikiana katika shughuli za maendeleo”. Alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mwanamvua Mlindoko, alisema wamejipanga kukamilisha ujenzi wa maabara katika shule za sekondari 15 ambapo kila shule zitajengwa maabara tatu ambazo jumla zitakuwa maabara 45.
Chanzo;Tasnzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa