Home » » WANAFUNZI 70 WANUSURIKA KIFO

WANAFUNZI 70 WANUSURIKA KIFO

WANAFUNZI 70 katika Shule ya Msingi ya Filbertbay iliyopo Kwamatiasi wilayani Kibaha, Pwani, wamenusurika kifo baada ya moto mkubwa kuzuka ghafla katika bweni pamoja na majengo mengine ya shule hiyo.
Tukio hilo lilitokea saa nane usiku wa kuamkia Novemba 11, ambapo uliteketeza kabisa mabweni ya wanafunzi, chumba cha kulia chakula, maktaba na miundombinu nyingine ya shule hiyo.
Wanafunzi hao wamenusurika baada ya jitihada za uongozi wa shule hiyo kufanikiwa kuwanusuru licha ya kutokuwepo gari la zima moto.
Akithibitisha kutokea kwa moto huo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema, moto huo umezuka ghafla katika bweni namba nne la wasichana.
Matei alisema, moto huo ulianza na kusambaa kwa kasi ambapo pia uliteketeza bweni lingine la wavulana, madarasa 14 ya kawaida, ofisi moja, maktaba, ukumbi wa chakula na darasa moja la Compyuta na maeneo mengine ya mazingira ya shule hiyo.
Taarifa za awali kutoka kwa kamanda huyo zinabainisha kuwa, chanzo cha moto huo ni hitirafu ya umeme na kwamba uchunguzi unaendelea.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Filbet Bay alikiri moto kuteketeza majengo hayo na kuongeza kuwa kwa sasa ni mapema mno kueleza thamani halisi ya madhara yaliyopatikana.
Tukio hilo la Moto limetokea siku mbili tangu tukio jingine kutokea na kuteketeza maduka katika eneo la Mailimoja mjini Kibaha huku gari la zimamoto likidaiwa kuwa katika matengenezo na hivyo kutegemea gari kutoka jijini Dar es Salaam
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa