MADUKA nane katika mji wa Mailimoja Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani yameteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wamiliki wa maduka hayo.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa mbili usiku na kusababisha taharuki kwa wakazi wa mji huo kutokana na kutoa mwanya kwa baadhi ya watu kutumia nafasi hiyo kupora baadhi ya mali zilizokuwa zikiokolewa na wasamaria wema.
Moto huo ambao chanzo chake hakijafahamika, ulianzia kwenye moja ya maduka hayo kabla ya kusambaa maduka mengine na kushika kasi kutokana na ‘fremu’ kuunganishwa huku juhudi za kuzima zikigonga mwamba kutokana na kasi ya uwakaji wake.
Kutokana na moto huo kusambaa kwa kasi huku gari la zimamoto likiwa halijafika eneo la tukio, nguvu za wananchi kuuzima moto huo zilikwama na kuamua kuendelea kujaribu kuokoa mali zilizokuwa kwenye maduka hayo huku kasi ya uporaji ikiongezeka.
Kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu, ambao walionekana kukimbilia kunawa maji usoni na kunywa kisha kurudi tena eneo la tukio na kuendelea na uporaji.
Mmoja wa wamiliki wa duka jirani na yaliyoteketea, William Felix, alisema wapo watu waliokuwa wakijidai ni wasamaria wema, walisimama nje ya ofisi yake wakati akitoa vitu ili moto ukisambaa usitekeze mali zake, walichukua maboksi na kutoweka kusikojulikana.
Gari la zimamoto lilitokea wakati vitu vikiwa vimekwishateketea, hali iliyowafanya wananchi kuhoji kama liko kwa ajili ya uokoaji au kushuhudia moto ulivyoteketeza mali, kwani moto huo ulipoanza simu ilipigwa ili kupata msaada wa gari hilo.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Pwani, Zelote Urio, alisema kuwa gari la zimamoto la kituo chao ni bovu, hivyo walilazimika kuwasiliana na uongozi wa Jiji la Dar es Salaam kupata msaada, hali iliyochangia kuchelewa kufika eneo la tukio.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na uchunguzi bado unaendelea.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment