Home » » TAMISEMI:HATUJAAGIZA WATUMISHI KUKATWA MISHAHARA KWA AJILI YA MAABARA

TAMISEMI:HATUJAAGIZA WATUMISHI KUKATWA MISHAHARA KWA AJILI YA MAABARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu), Kassimu Majaliwa (pichani), amesema serikali haijaagiza wakurugenzi kukata mishahara kwa watumishi kwa ajili ya ujenzi wa maabara nchini.

Akizungumza juzi wakati wa kukabidhi majengo yaliyojengwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama) katika Shule ya Sekondari Nyamisati, wilayani Rufiji, mkoani Pwani, alisema michango hiyo ni hiyari na siyo lazima.

“Haizuiliwi watumishi kuchangia miradi ya maendeleo, ni wajibu wa viongozi husika kuwaomba, serikali haijawatuma Wakurugenzi kuwakata watumishi mishahara yao kwa ajili ya ujenzi wa maabara,” alifafanua.

Ufafanuzi wa Waziri huyo umekuja wiki chache baada ya NIPASHE kuibua suala la Waratibu Elimu kata na Watendaji, kutakiwa kukusanya michango kutoka kwa walimu huku ikiweka bayana viwango kulingana na ngazi ya mashahara.

Mkoani Tanga, baadhi ya Halmashari nyingine wakuu wa idara wanatakiwa kutoa bati mbili na Sh. 25,000 kila mmoja na watumishi wengine wakiwekewa viwango tofauti tofauti.

Mkoani Kilimanjaro, wazazi wenye watoto wa kidato cha kwanza wanachangia 30,000 na kidato cha pili hadi sita kiasi cha Sh. 20,000 na wakuu wa shule wamepewa barua za maelekezo kutoka kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Kwa mujibu wa barua ya Septemba 15, mwaka huu, kutoka moja ya Halmashauri nchini (jina limehifadhiwa) kwenda kwa waratibu wa elimu wa kata, ikiwa na kichwa cha habari cha Michango ya maendeleo kuchangia ujenzi wa maabara, imewataka waratibu hao kukusanya fedha hizo kutoka kwa walimu.

Aidha, barua hiyo ambayo NIPASHE imeiona nakala yake, imeeleza kuwa kulingana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya ukamilishwaji wa maabara katika shule zote za sekondari nchini, uongozi wa halmashauri umeridhia uchangiaji huo.

“Kwa barua hii naagiza uchangiaji wa ujenzi wa maabara kutokana na maamuzi ya wilaya,” ilifafanua barua hiyo.

Barua hiyo ilifafanua viwango vya uchangiaji kuwa ni waratibu elimu kata Sh 60,000, walimu ngazi ya mshahara TGTS F-G Sh 60,000, ngazi ya mshahara TGTS D-E Sh 30,000 na TGTS B-C Sh. 20,000.

Aidha, barua hiyo ilieleza kuwa michango hiyo itatolewa kwa awamu mbili Septemba na Oktoba, mwaka huu.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa