Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wiki hii, Kampuni ya Mwananchi COMMUNICATIONS Ltd, inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen, imejitosa kudhamini tamasha la kwanza kubwa la sanaa litakalofanyika Bagamoyo Pwani, linalojulikana kwa jina la Karibu Arts and Music Festival.
Kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, wasanii wengi wamekuwa wakiomba kushiriki tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Novemba 7 hadi 9 mjini Bagamoyo, ambapo jana orodha ya kwanza ya wasanii waliokidhi vigezo vya kushiriki tamasha hilo imetolewa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, meneja wa tamasha hilo, Richard Lupia (Pichani), alisema kuwa wanatarajia wasanii wengi zaidi watajitokeza kushiriki Karibu Arts and Music Festival.
Alisema kuwa tamasha hilo limeanzishwa mwaka huu ambapo linatarajia kushirikisha wasanii mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Lupia alisema kuwa hadi sasa idadi ya walioomba kushiriki inaonyesha dhahiri kuwa watakuwa wasanii wengi ingawa mwaka huu ni mara ya kwanza tamasha hilo kufanyika.
Alisema kuwa wameandaa tamasha hilo kwa lengo la kukuza utamaduni na utalii nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.
Alitaja wasanii wa kimataifa waliothibitisha kushiriki kuwa ni pamoja na Panda(Japan), Maria Kate(Ufaransa), IFE Pianki(Uganda), Masayo(Japan), Fantuzz(Marekani), Shiwe Musique(Comoro), Dwmbede(Kenya) na Mbiye Ebrima(Guinea).
Makundi kutoka Tanzania ni pamoja na Jhikoman & Afrikabisa Band, Wahapahapa, Segere Original, Barnaba, Vitalis Maembe, The Spirit Band, Mama Africa, Chibite Zawose, Afrikwetu, Tongwa Ensemble na Leo Mkanyia & Swahili Blues.
Wengine ni Cocodo Band, Hokororo Band, Lumumba Theater, Mswanu Gogo Vibes, Swahili Vibes, Fimbo Band, Abeneko Music, Man Kifimbo, Saganda na Msafiri Zawose.
“Lengo kuu la tamasha ni kusisitiza kurasimishwa kwa tasnia ya muziki na kuwa na umakini zaidi, lakini kingine ni kukuza uchumi wa eneo husika la Bagamoyo ambalo ni la kihistoria na kuhakikisha sanaa ya asili ya Mtanzania inaonekana katika jukwaa la kimataifa,”alisema Lupia.
Tofauti na matamasha mengine yaliyowahi kufanyika Tanzania Bara, Karibu Arts and Music Festival litatoa burudani kutumia ala kwa asilimia mia moja. Wasanii wote watakaoshiriki, watalazimika kupiga muziki kutumia ala na kuimba na siyo ‘Playback’.
Lupia alisema mbali na kutoa burudani, wasanii pia watapata nafasi ya kujifunza jinsi ya kuunadi muziki wao duniani kwa njia mbalimbali kwa kushiriki warsha zitakazoendeshwa na wataalamu tofauti kutoka pande zote za dunia
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment