Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAKAZI wa Kijiji cha Chamakweza Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambao wengi wao ni wafugaji wameweka kambi kwa muda usiojulikana wakipinga kijiji chao kuingizwa kwenye mipango mji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema Kijiji chao kilitengwa kuwa cha wafugaji tangu mwaka 1974, hivyo endapo kitaingizwa kwenye mipango miji itawalizimu kufuga kisasa jambo ambalo ni gumu kwao.
Kijiji hicho ambacho kina wakazi zaidi ya 4,500 wakiwa na ng’ombe 22,000, mbuzi 6,000 na kondoo 4,000, mipango miji ikianza wakazi wake watalazimika kufuga ng’ombe wasiozidi 10 kila mmoja.
Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho, Mbambile Kisanjo, alisema wameweka kambi kwa muda usiojulikana kupinga utaratibu wa mipango miji, ambao hawajashirikishwa na viongozi wa serikali wakati mikakati hiyo ikifanyika.
Samwel Mganga, alisema kuwa serikali ya awamu ya kwanza ndiyo iliyowapatia eneo hilo kwa ajili ya wafugaji, hivyo huo utaratibu mpya unaotaka kuanza hawakubaliani nao kwani ni wa kuwahangaisha kwa kuanza kuhama hama.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Pwani, Mohamed Leboi, alisema kuwa anaunga mkono pingamizi linalowekwa na wakazi wa Kijiji hicho kuingizwa kwenye mipango miji kwani litaathiri maendeleo yao na kuharibu mipango waliyojiwekea.
Alivitaja vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya wafugaji ambavyo vitakumbwa na adha hiyo kuwa ni pamoja na Lulenge, Ubena, Pera, Malivundo, Chamakweza na Bwilingu ambazo ni sawa na hekta 53,106.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Mikalain Lemwes, alisema kuwa mipango miji wanaihitaji kwa maendeleo, isipokuwa itakapoingia matumizi ya ardhi yatabadilika kutoka eneo la wafugaji na kuwa mji.
Diwani wa kata hiyo ambae ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shukuru Mbato, alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo, alisema atafanya mkutano na wakazi hao kuzungumzia suala hilo huku akikwepa kueleza ukweli kuhusiana na Kijiji hicho kuingizwa kwenye mipango miji.
chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment