Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WASHIRIKA katika makanisa mbalimbali hapa nchini wametakiwa
kuongoza katika harambee zinazofanywa kwenye makanisa yao na kuacha
kutegemea wafadhili pekee kuwafanyia mambo kama hayo ya maendeleo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Fedha wa kampuni T/MARC Tanzania,
Mark Rajabu, wakati wa hafla ya uchangiaji ujenzi wa kanisa la
Tanzania Assemblies Of God (TAG), Picha ya Ndege mjini Kibaha, mkoani
Pwani.
Rajabu ambaye alichangia sh milioni 8 kwenye harambee hiyo,
alisema, uchangiaji kwenye shughuli za maendeleo usitegemee zaidi
wafadhili, badala yake nguvu zaidi zitumike kwa wanaoandaa na wafadhili
wasaidie kukamilisha shughuli iliyolengwa ambayo itakuwa na manufaa
zaidi kwa wahusika.
“Kuchangia ujenzi wa kanisa ni moyo na si kama anayechangia ana fedha
sana, lakini pia wito wangu washirika waongoze kuonyesha njia katika
uchangiaji, ili hata mfadhili anapojitokeza anaongezea nguvu na si
kutegemea kila kitu cha kimaendeleo kufanywa na wafadhili,” alisema.
Aidha, Rajabu aliwaasa wananchi katika maeneo mbalimbali, kutumia
rasilimali walizo nazo, kusaidiana katika kufanikisha suala la kuleta
maendeleo kwenye maeneo husika badala ya kutegemea watu kutoka mbali
kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
“Wapo watoto wa mitaani, nao si kwamba wamependa kuwa katika hali
ile, kinachotakiwa kutoka kwetu ni upendo, kwa kila aliye nacho
kumsaidia mwingine badala ya kuwa na roho ya uchoyo na kuendelea
kuwaacha wateseke,” alisisitiza.
Alimpongeza Mchungaji wa kanisa hilo kwa hatua ya kuanza ujenzi wa
kanisa kubwa, ambalo kwa kushirikiana na waumini wake wameweza
kufikisha ujenzi katika hatua ya ‘rinta’ na kuomba wadau wengine
kuwaongezea nguvu kulikamilisha.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment