Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAKAMU Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),
Magnus Muhiche, amesema kuwa anashindwa kuwaelewa baadhi ya wachungaji
wanaotanguliza harambee za ununuzi wa magari badala ya kujenga
makanisa.
Askofu Muhiche, alisema baadhi ya wachungaji hao wamekuwa wakifanya
ibada zao kwenye nyumba za kupangisha na wanapopata waumini zaidi ya
50, wamekuwa wakikimbilia kufanya harambee ya ununuzi wa magari na si
kununua kiwanja na kujenga kanisa ili kuondoka kwenye kupanga.
Akizungumza wakati wa hafla ya uchangiaji wa ujenzi wa Kanisa la TAG
Picha ya Ndege, Kibaha ulioambatana na kuweka jiwe la msingi juzi,
Muhiche aliwaasa wachungaji vijana kuanza na ujenzi wa makanisa na
suala la nyumba na magari ni baraka za Mungu wakati wakiendelea na
ibada kwa kuwaongoza waumini wao.
“Mimi wachungaji vijana wa namna hii siwaelewi kabisa na sitakaa
kuwaelewa, kwani magari na nyumba ni kuzidishiwa kutoka kwa Mungu, ila
wapo wachungaji wapo kwenye nyumba za kupanga wanafanya ibada zao,
lakini wanapopata waumini 50 tu, wanafanya harambee ya kununua gari la
mchungaji na si kujenga kanisa,” alisema.
Awali akisoma risala ya kanisa hilo, Mchungaji Kiongozi Spear
Mwaipopo, alisema kanisa hilo lilianzishwa miaka 20 iliyopita, ambapo
pamoja na changamoto zinazolikabili, lakini limeweza kuzalisha
wachungaji 12 ambao wamefunguliwa makanisa ndani na nje ya Mkoa wa
Pwani.
Mwaipopo alisema ujenzi wa kanisa hilo unatarajiwa kugharimu sh
milioni 85, ambapo hadi sasa milioni 52 zimetumika katika ujenzi wa
ofisi pamoja na kanisa hilo kubwa ambalo limefikia hatua ya ‘linta’.
Katika harambee hiyo, zaidi ya shilingi milioni 2 taslimu
zilipatikana na ahadi sh milioni 19, ambazo kati ya hizo, mdau wa
maendeleo, Mark Rajabu, alichangia sh milioni 8 kwa ajili ya ununuzi wa
mabati ya kuezekea.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment