Home » » HOSPITALI WILAYA MKURANGA HAINA HUDUMA YA X-RAY

HOSPITALI WILAYA MKURANGA HAINA HUDUMA YA X-RAY

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Wakazi wa Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, wamelalamikia Hospitali ya Wilaya hiyo kwa kutokuwa na huduma za X-ray, hivyo kuwalazimu kwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam kupata huduma hiyo.
Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema hospitali hiyo kukosa huduma za X-ray kunawasababishia gharama za kwenda jijini Dar es Salaam kupata huduma hiyo.

“Tunapopata matatizo ya kuumia au kuumwa na kufika hospitalini hapo, tunaambiwa hakuna huduma hiyo na kuambiwa twende Muhimbili kwa ajili ya kupata huduma hiyo,” walisema wakazi hao.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani humo, Rwey Jamal, alisema hiyo haikutakiwa kuitwa hospitali na ilitakiwa kuitwa kituo cha afya.

Alisema alipopata ajali ya pikipiki, alifikishwa hospitalini hapo na kupatiwa huduma ya kwanza, lakini akashauriwa kwenda Muhimbili kwa ajili ya kupata huduma ya X-ray kwa kuwa haipo katika hospitali hiyo.

Jamal alisema alishangaa kuambiwa hivyo na madaktari wa hosipitali hiyo, kwa kuwa huduma hiyo ilitakiwa kuwapo kutokana na kuwa ndiyo hospitali kubwa na kiungo katika barabara za mkoa wa Kusini na ajali za mara kwa mara huwa zinatokea.

Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Francis Mwanisi, alithibitisha kutokuwapo kwa huduma hiyo na kudai kuwa wapo mbioni kuiweka.

“Ni kweli hapa hospitalini inapotokea mgonjwa anatakiwa kupatiwa huduma ya X-ray, huwa tunamwambia aende Muhimbili. Lakini hivi sasa tumejipanga na muda siyo mrefu huduma hiyo itaanza kutolewa,” alisema Dk. Manisi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa