Kama kawaida asubuhi kulipopambanzuka wanakijiji cha
Maisha Plus walifanya usafi katika maeneo yao na usafi wa kisima cha maji
wanachotumia wanakijiji hao. Hii ni kuhakikisha wanaishi katika mazingira safi
na salama na yenye kuvutia kijijini hapo. Kwa kuwa ni siku ya Jumapili
wanakijiji hao hutumia siku hii kufanya ibada, kutembeleana na kujualiana hali.
Baada ya kutoka kanisani wanakijiji walitumia fursa hii kwenda kumfariji mtoto
aliyepotelewa na mama yake ambaye ametoweka kijijini hapo katika mazingira ya
kutatanisha siku ya Jumamosi majira ya asubuhi na kumpatia kiasi cha shilingi
elfu tano na mia moja ya pole. Hii inaashiria ushirikiano na umoja uliopo
miongoni mwa wanakijiji cha Maisha Plus.
Wanakijiji walitawanyika na kuelekea katika kaya zao
ambapo kila mwanakaya alielekea kwenye shamba lake na kujishughulisha na kilimo
ili kukidhi mahitaji ya kaya zao. Ilipowadia nyakati za alasiri mtaalamu wa
kilimo Bi. Janeth Maro kutoka shirika la Kilimo Endelevu Tanzania lenye makao
yake makuu mjini Morogoro aliwatembelea wanakijiji cha Maisha Plus na kujionea
namna wanavyojishughulisha na kilimo na wanavyokabiliana na wadudu
wanaoshambulia mazao yao. Wanakijiji cha Maisha Plus walikuwa na shauku kubwa
ya kutaka kujifunza zaidi kutoka kwa mtaalamu huyo kwa kuwa bustani zao za
mboga mboga zinashambuliwa na wadudu waharibifu.
Mtaalamu wa
kilimo Bi. Janeth aliwaeleza wanakijiji umuhimu wa kilimo hai ambacho kinatumia
utaalamu wa hali ya juu kwa kuusoma udongo, kutumia mbinu za kurutubisha,
kudhibiti magonjwa na wadudu na kuwa na mimea yenye afya na yenye nguvu ambayo
haiwezi kushambuliwa na maradhi mbalimbali. Vile vile aliwasisitiza wanakijiji
umuhimu wa kutumia mbinu ya kuhifadhi maji ardhini kwa kulima matuta yanayozuia
maji ya mvua kwenda kasi na kuleta madhara kwenye mimea na hivyo kuifanya ardhi
iwe na unyevu unyevu muda wote kama Mama Shujaa
Elinuru Moses Pallangyo alivyokuwa anaeleza na kuonyesha katika bustani
yake iliyotumika kupata somo hilo.
Naye Mama Shujaa
wa Chakula Grace G.D Maumbuka hakusita kutoa uzoefu wake katika kilimo hai
anachojishughulisha nacho na kusema kuwa mara nyingi hupanda miti rafiki
shambani ambayo majani yake huoza kiurahisi na kutunza unyevu unyevu ardhini.
Vile vile alisisitiza kupanda mazao jamii ya kunde kwa kuwa inarutubisha udongo
na kutolea mfano wa zao la njegere lilivyokuwa na faida kubwa kwa mkulima.
Alisema zao la njegere halihitaji nguvu nyingi, si rahisi kushambuliwa na
wadudu linapokuwa kavu na mimea yake haizalishi wadudu shambani na baadaye
mimea hiyo hutumika kama mbolea.
Wanakijiji
walifurahishwa sana na maelezo ya mtaalamu wa kilimo na kuuliza maswali mengi
kwa kuwa walikuwa wana shauku kubwa ya kujua masuala mbalimbali hasa namna ya
kukabiliana na wadudu waharibifu wanaoshambulia mazao yao hapo kijijini. Baada
ya hapo wanakijiji walitawanyika na kuelekea katika kaya zao huku wengine
wakijadiliana kuhusu somo hilo.
0 comments:
Post a Comment