Home » » EKAMA DEVELOPMENT WATEMBELEA KIJIJI CHA MAISHA PLUS NA KUTOA SOMO

EKAMA DEVELOPMENT WATEMBELEA KIJIJI CHA MAISHA PLUS NA KUTOA SOMO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Siku hii ilikuwa ya furaha na ya kihistoria kwa wanakijiji cha Maisha Plus. Mambo mbalimbali mazuri na yenye mafanikio yameweza kuonekana kutokana na juhudi za wanakijiji hao na ushirikiano miongoni mwao waliouonyesha kwa kipindi chote.
 Kwanza kabisa kulikuwa na shindano lililoongozwa na Hilda Mashauri na Roselyn Kaihula kutoka EKAMA Development. Shindano hilo lilihusisha timu ya Mandela na Nyerere ambapo kila timu ilitakiwa ijibu maswali yanayohusu mabadiliko ya tabianchi kwa ufasaha na muda mfupi ili ipate kushinda. Katika shindano hilo timu ya Mandela iliibuka kuwa mshindi kwa pointi 8.5 huku timu ya Nyerere ikiwa na pointi 7.5. Zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi hao ikiwemo keki, kinywaji maarufu kinachotumika katika shughuli hasa za harusi shampeni, mayai na kuku wawili, mchele pamoja na viungo vya pilau.
  Kwa kweli timu ya Mandela ilifurahishwa sana ushindi ule kwani washiriki waliruka ruka hapa na pale kuonyesha ishara ya fuaraha yao.
 Furaha hii ilienda sambamba na Kantangaze Entertainment Band ya kijijini hapo ambapo bendi hiyo ilipata waimbaji na uongozi mpya ili kuongeza nguvu zaidi na kuendelea kutoa burudani kijijini.

Waliojiunga katika bendi hiyo ni pamoja na Mama Shujaa Elizabeth Simon, Grace Mahumbuka na Dorothy Pallangyo ambaye ni meneja mpya wa bendi hiyo kwa sasa.

 Pia Mama Shujaa wa Chakula walipata fursa ya kuelezea kilimo cha makinga maji kinachohifadhi maji na kilimo hai kinachotumia dawa na mbolea za asili na kuendelea kupata mazao bora.

 Naye Doroth Pallangyo alionyesha uzoefu wake wa kutengeneza majiko kwa kutumia mali ghafi zinazopatikana kijijini hapo. Jiko la kupikia limetengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi na jiko la kutuza joto na kusaidia kuivisha chakula bila kuungua limetengenezwa kutumia kikapu, kitambaa na maranda ya mbao. 

Wanakijiji wengi walipendezwa na majiko haya kwani unaweza kuacha chakula chako kikiiva taratibu wakati huo ukifanya shusghuli nyingine mbali na hapo nyumbani.

 Vile vile Mama Shujaa walikaa na kuongea na watoto wao kuhusinana na athari za ukeketaji kwa wanawake ikiwemo maambukizi ya UKIMWI na kinamama kupata shida wakati wa kujifungua.

Siku ilimalizika kwa tukio la kihistoria kwa wanakijiji cha Maisha Plus kwa mara ya kwanza wameanza kutumia jiko la gesi ya kutengeneza kwa jina la kitaalamu biogas. Iliwachukua takriban wiki sita kukamilisha ujenzi wa jiko hili wakiongozwa na mwalimu wao Richard Daniel. 

Siku hii ilikuwa ni ya furaha kwa kila mwanakijiji kwani wameweza kupiga hatua katika maendeleo ya kijiji chao.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa