Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kwa takriban siku tatu Watanzania hususan wa mikoa ya ukanda
wenye mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Pwani na Morogoro walikuwa katika
misukosuko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mfululizo katika maeneo
hayo.
Mvua hiyo iliyobashiriwa mapema na Mamlaka ya Hali
ya Hewa (TMA) imesababisha maafa kwenye maisha ya watu, uharibifu wa
mali na hata miundombinu ikiwamo barabara na madaraja. Tunatumia nafasi
hii kuwapa pole wale wote ambao wameathiriwa na mvua hizo
zilizosababisha pia hasara ambayo hadi sasa ni vigumu kuitathmini.
Pamoja na madhara kwa mtu mmoja mmoja au jamii kwa
jumla ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya wananchi wakiwamo
wanaoishi mabondeni au maeneo hatarishi wakiendelea kupuuza miito na
hata tahadhari zinazotolewa, huku mamlaka zetu zikiwaachia waendelee
kuishi huko.
Kwa upande wao, tunatumia nafasi huu kuendelea
kuwasihi waondoke kwa hiari katika maeneo hayo kwani kulingana na TMA,
bado mvua hizo zinaweza kunyesha na hivyo kuwasababishia maafa na hasara
zaidi.
Pia tunatoa mkono wa pole kwa viongozi wetu,
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli na wengine wote walionusurika kwenye ajali ya helikopta
iliyotokea mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius
Nyerere wakati wakienda kukagua madhara yaliyotokana na mvua.
Hakuna shaka kwamba mvua hizo zitaigharimu
Serikali kiasi kikubwa cha fedha katika kurudisha miundombinu hiyo
katika hali yake ya kawaida. Tunaishauri serikali ifanye tafakuri ya
kina kuhusu sababu za mafuriko hayo na namna ya kuyaepuka. Tunaamini
zipo sababu za kibinadamu zilizochangia katika uharibifu huo wa
miundombinu na ambazo zingeweza kuepukika.
Kwa mfano, kingo za baadhi ya barabara
zimeathiriwa na ujenzi holela uliofanywa na wananchi huku mamlaka zetu
zikiwatazama na hivyo kusababisha mmomonyoko ambao hatimaye husababisha
barabara au madaraja kubomoka wakati wa mvua.
Aidha, wapo wananchi katika maeneo mengi ambao kwa
makusudi wanaziba mifereji au mitaro ya maji ya mvua, kutupa taka
kwenye madaraja, kiasi kwamba imekuwa rahisi kwa mvua kusomba na
kuathiri miundombinu.
Tunaishauri Serikali, hasa Wakala wa Barabara
(Tanroads) na mamlaka nyinginezo zikiwamo halmashauri zote, zichukue
hatua za makusudi kuzuia kutokea tena kwa mambo kama hayo yanayoitia
hasara nchi kwa kiasi kikubwa pia kupoteza maisha ya watu kama ambavyo
imetokea kwenye mvua zilizonyesha siku chache zilizopita.
Tunashauri hatua zinazostahili zichukuliwe
zikiwamo za kutunza mazingira kwenye miundombinu kama vile kuzuia ujenzi
holela na uharibifu wa mazingira. Pia, tunaiomba Serikali itafute njia
mbadala za kuepusha madhara yanayosababishwa na kufungwa kwa barabara
kuu zinazoingia Dar es Salaam, Morogoro, Bagamoyo na Kilwa juzi na hivyo
kusababisha usumbufu na hasara kiuchumi.
Njia hizo ni pamoja na kufufua reli ya kati na
Tazara, kuhakikisha ujenzi wa barabara imara zitakaoifanya Dar es Salaam
kuondokana na uwezekano wa kuwa kama kisiwa, kutekeleza mpango wa
kujenga bandari za nchi kavu kuepusha athari za magari kwa barabara.
Kwa kufanya hivyo, tunaamini matatizo haya yatapungua kwa kiasi kikubwa.
reli hizi zitatumika kusafirisha shehena, abiria ukiwamo wakati wa dharura na hivyo kuokoa maisha, fedha ambazo zinapotea kwa kufungwa kwa miundombinu yetu.
Chanzo:Mwananchi
reli hizi zitatumika kusafirisha shehena, abiria ukiwamo wakati wa dharura na hivyo kuokoa maisha, fedha ambazo zinapotea kwa kufungwa kwa miundombinu yetu.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment