RAIS
Jakaya Kikwete, jana ameshuhudia msururu mkubwa wa magari na maelfu ya
wasafiri waliokwama katika eneo la Ruvu Darajani, mkoani Pwani, kutokana
na kasi kubwa ya maji yanayopita juu ya daraja hilo.
Hali hiyo
inatokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali
nchini, kusababisha maafa kwa wananchi pamoja na uharibifu wa
miundombinu hususan madaraja.
Miongoni mwa watu waliokwama eneo hilo
ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bw. Job Ndugai
aliyekuwa akitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Dodoma.
Akizungumza
katika eneo hilo, Rais Kikwete alisema mafuriko hayo hayaepukiki ambapo
wajibu wa Serikali ni kuwasaidia waathirika, kwa taarifa alizonazo, 10
wamethibitika kupoteza maisha kutokana na mafuriko hayo.
"Mvua hizi
zimekuwa na madhara makubwa kwani hata daraja la Bunju limebomoka na
kukata mawasiliano kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo.
"Kwa sasa
Serikali inaangalia uwezekano wa kufungua Barabara ya Mlanzidi-Bagamoyo,
kama kasi ya maji itapungua ili kupunguza msongamano wa magari,"
alisema.
Aliongeza kuwa, mafuriko hayo yamechangiwa na mvua ambazo
zinaendelea kunyesha kwenye Milima ya Uluguru, mkoani Morogoro na
kusabisha mito mingi kujaa maji.
Kutokana na hali hiyo, Rais
Kikwete, ameliagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kambi ya Ruvu,
kuhakikisha wasafiri waliokwama katika eneo hilo wanapata vyakula kwa
bei nafuu.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo baada ya kukuta sahani
moja ya wali inauzwa sh. 4,000 na kuwataka wananchi wachukue tahadhari
kwani mvua hizo bado zinaendelea kunyesha.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Mkoa wa Pwani, Bi. Mwantumu Mahiza, alisema hajawahi kuona mafuriko ya
aina hiyo. Mvua hizo ambazo jana zimeingia siku ya tatu mfululizo,
zimeendelea kuleta madhara kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wengine
wakikosa makazi.
Baadhi ya watu wamekuwa wakitafuta ndugu zao bila mafanikio kutokana na nyumba walizokuwa wakiishi kuzingirwa na maji.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment