WANANCHI wa Kijiji cha Vikumburu Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani
wanaziomba kampuni za simu za mikononi kuwapelekea huduma ya
mawasiliano.
Ombi hili lilitolewa mwishoni mwa wiki, katika mkutano wa kijiji
ulioitishwa na Mwenyekiti wao Rashid Simba kujadili na kupitisha sheria
za kulinda misitu.
Akichangia hoja Mjumbe wa Kamati ya Maliasili Said Mkwama alisema
sheria walizopendekeza kwa kushirikiana na wenzao wa Halmashauri ya
Kijiji ni nzuri lakini ulinzi wa kushtukiza utakuwa mgumu kutokana
kukosa mawasiliano.
“Sheria tulizotunga ni nzuri na zitafanikisha kutunza na kuilinda
misitu lakini tutashindwa kufanya ulinzi wa kushtukiza kwa kuwa hatuna
mawasiliano ya mtandao wowote … hivyo tutaibiwa maliasili zetu,”
alisema Mkwama.
Naye Seleman Dude alisema hivi sasa wanalazimisha mtandao wa Airtel
kwa kupanda juu ya miti eneo moja porini ambalo waliliteua kwa ajili ya
kupata mawasiliano.
Kutokana na hali hiyo ya kukosa mawasiliano, Dude alitoa rai kwa
Mwenyekiti wa Kijiji kwa kushirikiana na viongozi wengine kufanya
jitihada za kuwaombea mtandao katika kampuni mbalimbali za simu nchini
ili nao waingie katika teknolojia.
Diwani wa Kata ya Vikumburu, Rashid Dihomba (CUF), alisema suala la
kuwatafutia mtandao wa mawasiliano amelifanya kwa muda mrefu bila
mafanikio hali inayomfanya atafsiriwe vibaya na wananchi wake.
“Inaniuma sana kuona wananchi hawanielewi pale ninapowaambia kwamba
nafuatilia kampuni mbalimbali za simu ili zituletee mtandao wa
mawasiliano, sitakata tamaa nitaendelea hadi kieleweke,” alisema
Dihomba
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment