Home » » Serikali yaahidi kuendelea kuiunga mkono Rubada

Serikali yaahidi kuendelea kuiunga mkono Rubada

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (Rubada), Aloyce Masanja (katikati) pamoja na Wajumbe wa Bodi ya mamlaka hiyo, Eline Sikazwe (kulia) na Jacob Muhumba (kushoto), wakifuatilia maelekezo kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kilombero Plantation Ltd (KPL), Graham Anderson, wakati wa ziara yao waliyoifanya katika shamba hilo lililopo eneo la Mngeta Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro,mwishoni mwa wiki.
 
Serikali imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (Rubada) kuhimiza uwekezaji mkubwa katika kilimo ili kuongeza tija katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.
Ahadi hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Raphael Daluli, katika shamba la kampuni ya KPL lililopo Mngeta katika Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.

Daluli alikuwa mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Rubada iliyofanya ziara katika shamba hilo kubwa la mpunga.

“Kwa kweli hii ni kazi nzuri, uwekezaji kama huu ndiyo unahitajika, shamba ni kubwa, mpunga umestawi, napenda kuwapongeza Rubada,” alisema.

Alisema teknolojia inayotumika katika kuandaa shamba mpaka kuja kukoboa mpunga ni ya hali ya juu sana na weledi na kuwa hiyo ndiyo inayotakiwa katika kuendeleza sekta hiyo kwa uwekezaji mkubwa kama huo.

Serikali yaahidi kuendelea kuiunga mkono Rubada


“Tumetembelea maeneo mengi sana, mfumo wa upandaji, umwagiliaji mpaka katika mashine za kukobolea ni za kisasa kabisa, hivyo tunahimiza wawekezaji wengi wa namna hii wajitokeze katika sekta hii ambayo kwetu ndio mkombozi,” aliongeza.

Mhandisi Daluli alisisitiza na kuhimiza kutumika kwa mfumo wa kilimo shadidi ili kuongeza idadi ya wakulima wanaozunguka katika shamba la Mngeta, kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza idadi ya watu tegemezi katika kaya.

“Nimeambiwa kuwa kuna mfumo wa kilimo shadidi, (SRI) ni kitu kizuri, ushauri wangu watu wa KPL na Rubada, wajitahidi kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo hili ili wauelewe na kujiunga,” alisistiza.

Akizungumzia suala la ajira katika shamba hilo, Naibu Katibu Mkuu huyo aliimwagia sifa KPL na kusema imefanikiwa kuwainua kiuchumi wananchi wa eneo hilo kutokana na kutoa ajira nyingi katika kiwanda hicho.

“Napenda kuwapongeza hawa wawekezaji, wengi wanabeza uwekezaji lakini kwa hali hii, huwezi kusita kuwaunga mkono kwa asilimia mia moja wanafanya kazi inaonekana na wananchi wanafaidika,” alisema.

Alisema huduma za jamii zilizopo katika eneo la Mngeta ni faida ya uwekezaji uliopo ambapo wananchi wamepunguza umbali wa kufuata huduma za afya baada ya kujengewa zahanati ya kisasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Rubada, Aloyce Masanja, aliishukuru bodi hiyo kukubali wito wa kwenda kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa katika shamba hilo.

Alisema kazi kubwa iliyoko mbele yao ni kuhakikisha wanaongeza maeneo mengine ya uwekezaji hasa yale yaliyo chini ya mamlaka ya hiyo.

“Hivi sasa tuna eneo la Ngalimila, ambalo tayari limeshapimwa na kilichobaki ni taratibu za uwekezaji kufanywa na watu kuanza kufanya kazi,” alisema Masanja.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa