Home » » Kidato cha pili Pwani wakithiri kwa utoro

Kidato cha pili Pwani wakithiri kwa utoro

Pwani.   Mkoa wa Pwani unakabiliwa na tatizo kubwa la wanafunzi wa kidato cha pili wanaotakiwa kukariri darasa kukimbia shule na baadhi ya wanaopangiwa kidato cha kwanza nao kutoripoti kabisa shuleni.
Kwa mujibu wa takwimu za Idara ya Elimu Mkoa, zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana, zaidi ya wanafunzi wa kidato cha pili 2,000 walishindwa kuendelea na masomo baada ya kufeli na kutakiwa kukariri darasa.
 Aidha, kwa upande wa wanafunzi waliopangiwa kidato cha kwanza mwaka jana huohuo, zaidi ya 2,600 hawakuripoti shule walizopangiwa na baadhi yao haikujulikana sababu kufanya hivyo.
 Hayo yamebainika katika kikao cha kupitia uchambuzi wa matokeo ya darasa la saba, ambapo wadau wa mkutano huo walionyesha kusikitishwa na hali hiyo ambayo wameeleza ikiongezeka kila mwaka.
Wakilalamikia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mecy Sila, Mbunge wa Jimbo la Kibiti Abdul Marombwa, Asha Itelewe na Shangwe Twamala walisema idadi ya wanafunzi wa kidato cha pili wanaokimbia shule baada ya kutakiwa kukariri darasa imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka tangu utaratibu huo ulipoanza.
“Wajumbe, hali ya watoto wetu kukimbia shule hasa kidato cha pili tunaichukuliaje, maana kundi kubwa linakimbia na wakuu wa shule wakiulizwa kutofahamu,” alisema
Pia baadhi ya wajumbe walilalamikia utaratibu wa usahihishaji mitihani ya kidato cha pili kuwa siyo mzuri kutokana na mitihani kutolewa mapema.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa