WATENDAJI katika ngazi mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya
ya Rufiji, mkoani Pwani, wametakiwa kuendana na kasi ya kazi katika
mfumo mpya wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili
kufanikisha mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Changamoto hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Uendelezaji Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Aloyce Masanja, mwishoni mwa
wiki katika semina ya kuwajengea uwezo madiwani, watendaji mbalimbali
katika ngazi za vijiji hadi tarafa juu ya mpango mpya wa usimamiaji na
ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ya serikali wa Matokeo Makubwa Sasa.
“Lazima mchague maeneo ambayo yataleta matokeo makubwa, lakini
vilevile nidhamu ya hali ya juu katika kufuatilia yale mliyoyapanga
kutekeleza kwa kipindi fulani, bila hivyo hatuwezi kufika,” alisema
Masanja.
Alisema ili nchi iweze kufikia katika malengo iliyojiwekea, ni lazima
viongozi wawe na uthubutu wa kujiwekea malengo katika utekelezaji wa
mipango yao katika maeneo yao na kushinda woga wa kushindwa.
Alisema katika mfumo mpya wa Matokeo Makubwa Sasa kila mtu atapimwa
kulingana na kazi anayofanya na atakayeshindwa atawekwa pembeni na
kuwaachia wale watakaoweza kumudu kazi husika.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu, aliwataka watendaji hao kutoa
ushirikiano kwa RUBADA, ili malengo yaliyowekwa na serikali ya mpango
wa Kilimo Kwanza uweze kufanikiwa.
“Ndugu zangu, sisi sote ni mashahidi, hakuna asiyeona kazi kubwa
inayofanywa na RUBADA katika kusimamia mpango wa kilimo katika eneo la
Rufiji, tusipofanya hivyo tutabaki nyuma siku zote,” alisema Babu.
Aliongeza kuwa Wilaya ya Rufiji kwa sasa haina viwanda, na kwamba
mkombozi pekee aliyebaki ni kujitahidi kuwekeza katika kilimo.
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment