Home » » ‘Dhana ya Mwenge wa Uhuru wengi hawaijui’

‘Dhana ya Mwenge wa Uhuru wengi hawaijui’



Pwani

ELIMU kuhusu umuhimu na maana halisi ya kuwepo kwa mbio za mwenge nchini kila mwaka imeelezwa kuwa ni vema ikatolewa kwa jamii kuanzia ngazi ya familia kwani hivi sasa kizazi kilichopo kimekuwa kikipuuzia uwepo wa mbio hizo kutokana na kutokuwa na ufahamu wake.

Hayo yameelezwa na kwa nyakati tofauti mkoani humo na baadhi ya wananchi  waliokuwa wakijitokeza kushuhudia mbio za mwenge wa uhuru ukifanya shughuli za kukagua,kuzindua na kuweka mawe ya msingi miradi mbalimbali katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe, Mkuranga na Rufiji mkoani humo ambapo katika maeneo mengi kundi la watoto wadogo na wanafunzi ndilo limekuwa likionekana linajitokeza zaidi kuushangilia mwenge likifuatiwa na wazee kadhaa na vijana wakiwa wachache tu.

Mashaka Musa, Azizi Jonh,Yusufu Kazikulinda na Bikidawa Halfani walipoulizwa kuhusu sababu za watu wazima wengi kutoonekana kushabikia mbio hizo ma wilayani na badala yake wamekuwa wakionekana watoto wengi zaidi walisema hiyo inatokana na kizazi cha sasa kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa mbio hizo za mwenge.

Wameiomba Serikali kupitia kitengo husika kinachoshughulikia masuala ya mwenge kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia na wanafunzi  juu ya umuhimu wa mbio za mwenge ili kuwajengea uelewa mpana vijana kizazi cha sasa na pia kuwafanya wazelendo wa Taifa lao.

Katika mbio hizo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Juma Simai mara kadhaa kwenye mikutano yake mkoani humo amekuwa akisisitiza suala la jamii kuwa wazalendo na mbio hizo za mwenge na pia waendelee kuuenzi kwa kuhamasishana kubuni,kuchangia na kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Hata hivyo Simai ameongeza kuwa mbio hizo zilianzishwa kwa falsafa ya kuhamasisha ukombozi wa taifa la Tanganyika na bara zima la afrika kama alivyosema baba wa taifa hayati Mwl Julius Nyerere na hivyo si vema kuubeza kama ambavyo baadhi ya watu wachache wanafanya bali sasa wauenzi kwa nguvu zote.

Mbio za mwenge mkoani Pwani  inahitimishwa Septemba 3 huko wilayani Mafia na kwamba katika mbio hizo umeweza kutembelea na kukagua miradi ,kuweka mawe ya msingi,kuzindua na kufungua na hadi unakamilisha mbio zake jumla ya miradi 65  yenye thamani ya sh. Bilioni 6.5 imepitiwa katika wilaya zote sita za mkoa huo.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa