Home » » Chama cha Afya ya jamii chaweka mikakati mipya kutatua kero za afya Pwani

Chama cha Afya ya jamii chaweka mikakati mipya kutatua kero za afya Pwani


Pwani

CHAMA cha Afya ya jamii nchini (TPHA) tawi la mkoa wa Pwani kimetakiwa kufanya kazi zake huku ikibuni mikakati mipya ya kutatua kero za afya zilizopo kwa jamii hasa kwa magonjwa yanayoepukika mipango ambayo kila wakati itakuwa inaendana na mabadiliko ya mazingira yaliyopo.

Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa chama hicho Taifa Elihuruma Nangawe kwenye uzinduzi wa tawi la TPHA Pwani shughuli ambayo ilifanyika jana kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo.

Nangawe amesema utendajimagonjwa yanayoweza kuepukika hayana sababu kuendelea kuwaandama watu katika miaka 50 ijayo huku wataalamu wa masuala ya afya wapo na hivyo ameshauri wanachama hao ambao wengi wao ni wataalamu wa afya wa fani tofauti wawaelimishe wananchi mkoani humo namna ya kuziepuka maradhi hayo kwani kinga ni bora kuliko tiba.

Nangawe amesema wanachama wanapaswa kutambua kuwa uwepo wa chama hicho pamoja na mambo mengine ni kutetea afya ya jamii kwa njia ya ushawishi,kupeleka habari sahihi ambayo itawasaidia wadau wa masuala ya afya nao kupata taarifa zilizopo ndani ya jamii ili wayafanyie kazi na kusaidia kuleta mabadiliko chanya.

Ametaja baadhi ya vipaumbele ambavyo kwa jamii ya mkoa wa Pwani itakuwa ni vema tawi hilo likaanza kuyatafutia uvumbuzi kwa njia ya ushawishi kuwa ni pamoja na masuala ya ajali za barabarani,dawa za kulevya, matende na madusha, kisukari na magonjwa mengineyo.

Awali katibu wa TPHA Taifa Oberlin Kisanga akielezea baadhi ya mambo waliyofanikiwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1980, alisema wao wameweza kutetea jamii katika masuala chanjo,madhara ya tumbaku,unywaji wa vilevi vya viroba kwa madereva ambapo wametoa ushawishi kwa wadau wa afya na Serikali imeshaanza kuyafanyia kazi matatizo hayo kwa kutoa chanjo kwa watoto na kuelimisha wananchi katika matangazo mbalimbali.

Kwa upande wao wanachama wa tawi hilo mkoani humu kupitia kwa katibu muenezi Feliciana Mmasi walisema wamekuwa na kiu muda mrefu wa kupata tawi mkoani humo ili kuwarahisishia utendaji kazi ambako sasa nguvu zaidi wataanza kuzielekeza katika kutoa ushawishi kwa magonjwa ambayo si ya kuambukiza kama kisukari, kansa, moyo na makundi maalumu juu ya madhara ya dawa za kulevya, ajali za pikipiki na ajali za barabarani mkoani Pwani.


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Pwani Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa