WANAFUNZI 58 waliochaguliwa kujiunga na Shule ya
Sekondari Visiga, mkoani Pwani wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na
kutembea umbali mrefu.
Wanafunzi hao wakazi wa Kata ya Mbwawa, Wilaya ya
Kibaha Mjini, walikatisha masomo miaka miwili iliyopita kutokana na kutomudu
kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 13 kutoka Kijiji cha Miswe hadi Visiga
ilipo shule.
Akielezea tatizo hilo kwenye mkutano wa kukabidhi
mashine za umwagiliaji, ulioandaliwa na Mbunge wa Kibaha Mjini Sylvestry Koka,
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbwawa, Ntizesa Ntirugelegwa, alisema idadi hiyo ya
wanafunzi waliokatisha masomo imetokana na kukosekana kwa sekondari ya kata.
Ntirugelegwa alisema katika kata hiyo kuna shule ya
sekondari ya kata ambayo imejengwa mwaka 2012 lakini hadi sasa haijakamilika
kutokana na kukosa vyoo na pia kuwepo na vyumba viwili tu vya madarasa.
Alitaja changamoto nyingine ni ukosefu wa shule za
msingi mbili katika mitaa ya Mkoleni na Miswe Chini, hali inayosababisha watoto
kutembea umbali wa kilomita tatu kwenda mitaa ya Mbwawa shule na Miswe Duka.
Mtendaji huyo alimuomba mbunge kusaidia kufanikisha
ujenzi wa shule za msingi katika mitaa hiyo pamoja na ujenzi wa vyoo katika
shule ya sekondari ya kata ambavyo hadi kukamilika vitagharimu sh milioni tano.
Akizungumza na wananchi hao, Koka alisema
alimuagiza mtendaji kuandika barua ya kuelezea changamoto za shule hiyo ya
sekondari ili aweze kufanya ufuatiliaji kwa mkurugenzi na shule hiyo ikamilike
mwishoni mwa mwaka huu ili mwakani wanafunzi waanze kuitumia.
Mbunge huyo alikabidhi mashine za umwagiliaji tano
zilizogharimu sh milioni 3 kwa vikundi vya vijana vya Miswe Kibaoni, Miswe
Duka, Miswe Chini, Mbwawa Shuleni na Mbwawa Mkoleni.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment